Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Mei 6, 2023) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya hayati Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Amesema kuwa kama lilivyo lengo la kongamano hilo ni muhimu kuwarithisha vijana wa Kitanzania fikra na falsafa za Baba wa Taifa. “Aidha, nyote mtakubaliana nami kwamba yapo mambo mengi ambayo tungetamani vijana wetu wayafahamu kuhusu urithi aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema baadhi ya mambo ambayo vijana wanapaswa kurithishwa ni kuyafahamu maisha ya Mwalimu Nyerere hasa baada ya kustaafu uongozi wa nchi na siasa za majukwaani, kutambua juhudi zake katika harakati za kuleta amani na kufanikisha ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na bara la Afrika.
Ameyataja masuala mengine kuwa ni kufahamu kipaji cha Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kupigania uhuru na kuwaunganisha Watanzania na kuwa na uwezo wa kumfahamu na kumuelezea Mwalimu Nyerere alikuwa ni nani katika historia ya Tanzania.
“Miongoni mwa urithi huo ambao tungependa kizazi chetu kiufahamu ni pamoja na kuwa na uwezo wa kumfahamu na kumuelezea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni nani katika historia ya Tanzania; kuzielewa na kuzitambua juhudi za zake katika kuimarisha ustawi wa Tanzania hususan kupitia falsafa yake ya kutokomeza maadui watatu yaani ujinga, umaskini na maradhi.”
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kumekuwa na taarifa za malalamiko kuhusu kuongezeka kwa kelele na mitetemo katika sehemu mbalimbali nchini na maeneo yaliyoongoza kwa kulalamikiwa ni za nyumba za starehe, kumbi za burudani na nyumba za ibada.
Amesema katika kudhibiti kelele na mitetemo kutoka katika kumbi za starehe, Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa maelekezo mahususi yaliyolenga kudhibiti mitetemo iliyopitiliza katika kumbi za starehe hapa nchini. Pia, maelekezo hayo yaliainisha jinsi uratibu unavyopaswa kufanyika katika nyumba za ibada kwa kuwaomba viongozi wa dini kupitia Kamati za Amani kujadili suala la kelele na mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha shughuli za ibada.
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema, kumejitokeza taharuki kwa baadhi ya viongozi wa dini wakati Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashughulikia malalamiko kuhusu ongezeko la kelele na mitetemo.
“Serikali ingependa kutoa ufafanuzi kwamba shughuli za dini ziendelee kufanyika kama kawaida na suala la uratibu wa jambo hilo katika nyumba za ibada liendelee kuratibiwa na viongozi wa dini wenyewe kupitia Jumuiya ya Maridhiano na Amani.”
“Serikali itaendelea kushauriana na jumuiya ya maridhiano na amani katika kuona namna bora ya kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na kulinda afya za Watanzania,” amesema.
Mapema, Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa Watanzania kuyaishi maono ya hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na kuwa wazalendo kwa kuwa mwalimu Nyerere bado anaishi kutokana na falsafa zake alizoziacha kwa Taifa.
Naye, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu amesema kazi za hayati Mwalimu Nyerere zitakumbukwa milele na milele kwani ni mtu muhimu kwa Taifa letu. “Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kupitia kongamano hili ndicho chombo kitakachoweza kuwasaidia vijana kufahamu nini Mwalimu Nyerere alifanya, tofauti na hapo historia itapotea.”
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mzee Paul Kimiti ameiomba Serikali itenge eneo kwa ajili ya makumbusho ya hayati Mwalimu Nyerere katika makao makuu ya Serikali hapa Dodoma ambayo yatahifadhi historia yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amewasihi vijana wawe wazalendo kwa kuipenda Tanzania kwani uzalendo ni silaha muhimu sana katika kuliletea Taifa maendeleo.
Aidha, Mheshimiwa Pinda amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwawezesha vijana ikiwemo kuanzisha mpango wa kesho iliyo bora (Building a Better Tomorrow) wenye lengo la kuwawezesha vijana kwenye sekta ya kilimo.
No comments:
Post a Comment