Habari za Punde

Kumekuwepo na Changamoto Juu ya Matumizi ya Simu kwa Watoto Yanapelekea Kuibuka kwa Vitendo vya Udhalilishaji kwa Watoto.

Na Maulid Yussuf WMJJWW -Zanzibar. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amesema  kumekuwepo na changamoto juu ya matumizi ya simu kwa  watoto ambayo yanapelekea kuibuka kwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.

Mhe Waziri amesema hayo wakati akifungua kongamano la siku ya mtoto wa Afrika na siku ya kupinga ukatili kwa wazee, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Studio Rahaleo Mjini Unguja.

Amesema wamekuwa wakishudia wimbi kubwa la wazazi kuwaacha watoto kutumia simu za mkononi bila kuzingatia matokeo yanayoathiri makuzi na maendeleo yao, hivyo amesema ni lazima kila mzazi kuzingatia suala hilo.

Akizungmzia kauli mbiu ya mwaka huu ya " Muweze na mlinde mtoto katika matumizi sahihi ya Mtandao"  Mhe.Riziki amesema ujumbe huu umekuja wakati muwafaka kwani matumizi ya mitandao kwa watoto nayo yanachangia vitendo hivyo vya udhalilishaji. 

Amesema wanapoadhidhimisha siku ya Mtoto wa Afrika wanakuwa wakikumbuka watoto waliouawa kikatili Mjini SOWETO katika nchi ya Afrika ya Kusini mwaka 1976, wakipinga ubaguzi wa rangi na utumiaji wa Lugha ya Kikaburu (Africans) Maskulini.  

Aidha Mhe. Riziki amewapongeza viongozi  wa JUWAZA kwa kufikiria kuungana na Mataifa mengine ya Afrika katika siku hiyo kwa lengo la kutaka kuijuilisha jamii umuhimu wa Mtoto na Mzee katika Jamii. 

Amesema siku hiyo inatoa fursa kwa kuweka misingi mizuri ya kuwalinda na kuwaendeleza watoto  ili kujenga kizazi bora na chenye kuzingatia maslahi yao. 

Pia amesema siku hiyo inawapa msukumo wa kuzidisha mashirikiano baina ya wazazi, walezi, sekta zinazowahudumia mama na mtoto pamoja na mashirikiano na  wadau wa maendeleo katika kusimamia na kuitekeleza sheria Nam. 6 ya mtoto ya mwaka 2011, Zanzibar pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa inayohusu masuala ya mtoto. 

Akizungumzia masiku ya kupinga udhalilishaji wa Wazee, Mhe. Riziki amewaomba jamii kubadili mwenendo na tabia katika kuishi na wazee hasa kwa kuwafanyia wema na ihisani ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu na  kuneemeka hapa duniani na kesho siku ya hesabu. 

Amesema kumekuwa na tabia ambayo haikubaliki na haizoeleki kwa baadhi ya watoto kuwatelekeza wazee, kuwatolea lugha chafu (Udhalilishaji wa Hisia), na hata wengine kujaribu kutaka kufanya ukatili wa Kingono jambo ambalo katika utamaduni na imani  haukubaliki. 

"Napenda kutumia fursa hii kukumea na kulani vikali wale wote ambao wamekuwa wanawafanyia vitendo hivyo Wazee wetu, kwani wazee ni hazina na tunu ya Taifa kama wahenga wasemavyo “Utu uzima ni Dawa” Jee tunapowafanyia udhalilishaji matarjio yetu ya kupata nasaha au ushauri yatatoka wapi? Ametanabahisha Mhe. Riziki 

"Sipati raha sana pale ninapoona baadhi wa watoto wanawaacha wazazi katika makaazi maalumu kwa matarajio kwamba Serikali iendelee kuwahudumia wazee hao. Tutambue kuwa  bado ni jukumu la watoto kuendelea kuwahudumia Wazee wao mpaka pale hatma ya mwisho miongoni mwao itakapowafikia na sio kuwaweka wakiwa pweke mfano katika Makaazi ya Wazee Sebleni, Welezo au Limbani au kwa Watu baki" amesisitiza Mhe.Riziki .

Naye Mkurugenzi Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee bwana Hassan Ibrahim Suleiman amesema watoto na jamii kwa ujumla ni vyema kujua haki za wazee kwa ujumla kwani wao ndio nguzo muhimu ya kufika hapo walipo sasa.

Amewapongeza Jumuiya ya Wazee Zanzibar JUWAZA kwa kuona umuhimu wa  kuandaa kongamano hilo ambalo litajadili masuala mbalimbali ya  watoto na haki zao pamoja na kupinga ukatili kwa wazee nchini.

Kwa upande wake Katibu wa JUWAZA Bi salama Ahmed Kombo  amesema kumekuwa na udhalilishaji kwa baadhi ya wazee katika nyanja tofauti, hivyo ni  vyema kuwaelimisha  watoto juu ya masuala hayo pamoja na kujua haki zao.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa  katika nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika,  kila ifikapo Juni 16 ya kila mwaka,  ambapo katika kongamano hilo mada tatu zimewasilishwa ikiwemo, Wajibu wa jamii katika kumlinda mtoto kutokana na matumizi ya kidijitali,  Kuzeeka kwa afya na kulinda unyanyasaji kwa wazee pamoja na mada kuhusu Kinga mjumuisho katika makundi rika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.