Habari za Punde

Tanzania na Algeria Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria Ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Samwel Shelukindo akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika tarehe 30 Julai, 2023 jijini Algiers, Algeria.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza diplomasia ya uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi unaoendelea jijini Algiers, Algeria.

Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 31 Agosti 2023 ambapo kwa pamoja mikutano hiyo inafanya maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 1 Agosti 2023.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano ngazi Wataalam umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na kwa upande wa Algeria umeongozwa na Mkurugenzi Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Balozi Selma Haddadi Malika.

Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.

Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.

‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo.

Naye Mwenyekiti Mwenza, Balozi Selma Malika katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.

‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara, mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.

Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou ulilosababishwa na kuongezeka kwa joto kali. 

Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara, viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia, mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.