MAKAMU Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekiahidi chama hicho kufanya mkutano mkuu
wake Taifa ndani ya visiwa vya Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti
huyo aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Wenyeviti wa Chama hicho
wa mikoa yote ya Tanzania waliofika kumsalimia.
Alisema CCM Zanzibar,
itahakikisha inalifanikisha hilo kwa kuwezesha ufanisi wa rasilimali zote
ikiwemo eneo muafaka la kuhudumia wajumbe wote wa mkutano mkuu taifa pamoja na
mikutano mengine ya Halmashauri kuu taifa kwa kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano
ambao chama utajivunia nchi nzima ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Rais Dk. Mwinyi,
alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuwaalika viongozi hao wa chama
kuhudhuria Tamasha la Kizimkazi.
Aidha, alisifu ujio
wa viongozi hao kuwa ni njia moja ya ushirikiano na kudumisha umoja na mshikamo
wao ndani ya chama, hivyo aliwaomba viongozi hao kutembelea maeneo mengine na
kujionea miradi ya maendeleo ya chama hicho kwa kubadilishana uzoefu.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama Ndg.Talib Ali Talib
alimueleza Makamu Mwenyekiti huyo jinsi walivyoupokea ugeni huo na kuutembeza
maeneo mbalimbali ya historia ya Zanzibar ikiwemo, Hifadhi ya Mji Mkongwe wa
Zanzibar na kuangalia maeneo mengine ya Utalii.
Naye, Mwenyekiti wa
CCM, Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi kwaniaba ya wenyeviti wa chama hicho kwa
ngazi za mikoa yote nchini, walimpongeza Makamo Mwenyekiti Rais Dk. Mwinyi kwa
hatua kubwa ya maendeleo aliyoifanikisha ndani ya kipindi kifupi cha uongozi
wake.
Pia, Wenyeviti hao
walimshukuru Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mwaliko aliowapa kuhudhuria Tamasha la Kizimkazi na
kujionea mandhari halisi ya Zanzibar kwa waliokuwa hawajawahi kufika.
Walisifu hatua hiyo,
njia ya kukuza utalii wa ndani na kudumisha ushirikiano kwa viongozi wa chama
hicho wa mikoa yote nchini.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU - ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment