Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Balozi wa Israel nchini Tanzania, Mheshimiwa Michael Lotem, amesema kuwa Sekta Binafsi nchini mwake iko tayari kuwekeza mitaji, ujuzi na teknolojia katika sekta mbalimbali kikiwemo kilimo, TEHAMA, huduma za jamii pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Lotem amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lamck Nchemba Madelu (Mb), katika Ofisi za Hazina Ndogo, Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa Tanzania ina ardhi kubwa na yenye rutuba ikilinganishwa na nchi nyingine za jirani, hatua iliyowavutia wawekezaji wengi kutoka nchini Israel kutaka kuja kuwekeza nchini, hatua itakayokuza tija katika kilimo, kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni
Mheshimiwa Lotem, alisema kuwa kwa upande wa Serikali ya Israel, iko tayari kutoa mbegu bora za mazao ya kilimo pamoja na teknolojia zake za uzalishaji hatua itakayoiwezesha Tanzania kutimiza malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula na kulisha nchi nyingi duniani kupitia kilimo cha umwagiliaji.
Alibainisha pia kuwa kampuni hizo za Israel zinazotaka kuwekeza nchini baada ya kuridhishwa nah atua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji, ziko tayari kuja na mitaji yao bila kutegemea dhamana za serikali kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miradi husika.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa Tanzania iko tayari kunufaika na ujuzi wa aina mbalimbali hususan katika sekta ya kilimo kutoka nchini Israel kwa kuwa agenda ya kilimo ndiyo inayopigiwa chapuo hivi sasa kwa nguvu zaidi nchini, chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa kutokana na kutambua umuhimu wa sekta hiyo ya kilimo, Serikali imeongeza bajeti yake kutoka shilingi bilioni 250 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni moja kwa kuwa inagusa sehemu kubwa ya maisha ya watanzania na kuwa chanzo cha ajira ya uhakika kwa vijana.
Alisema pia kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuitumia Sekta binafsi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na kuwaalika wawekezaji hao kutoka Israel kuja kuwekeza nchini na kwamba Serikali iko tayari kuwapatia ardhi ya kuendesha shughuli za kilimo ambacho pia kitakuwa shamba darasa kwa watanzania wengine.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Meneja Mkazi wa Kampuni ya ujenzi ya Reynolds kutoka nchini Israel, Mhandisi Ronen Gershon.
No comments:
Post a Comment