Habari za Punde

Tabia aufungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana Zanzibar

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo  Mhe, Tabia Maulid Mwita akifungua Mkutano  Mkuu  wa Baraza la Vijana Zanzibar hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla  akiwashauri vijana kujiunga katika mafunzo ya ujasiriamali ili kuweza kujiajiri hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.

Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo  pamoja na Baraza la Vijana wakisikiliza kwa makini maelezo yanayotolewa na Waziri wa Wizara hiyo  Mhe, Tabia Maulid Mwita(ambae hayupo pichani)  katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana uliofanyika  Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.

 PICHA NA YUSSUF SIMAI  MAELEZO


Na Rahma Khamisi Maelezo   14/9/2023

 

Waziri wa Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo Mhe.  Tabia Maulid Mwita amewataka vijana kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuleta maendeleo nchini.

 

Akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Vijana Zanzibar  katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo amesema ni vyema vijana  kujishughulisha na kazi za ujasiriamali wa aina mbalimbali ili kufikia malengo ya kujiletea maendeleo.

 

Aidha amesema iwapo vijana watajituma na kufanya kazi kwa  bidii na uzalendo watasaidia kuimarisha maendeleo yaliyopo katika jamii.

 

 Waziri Tabia amewaasa vijana kuacha kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake kujishughulisha na kazi za mikono kwa kujiongezea kipato.

 

"Sisi vijana tunaangaliwa na viongozi wetu hivyo ni vyema tukasimamia yale tunayopewa ili tuweze kutatua changamoto zinazotukabili," alisisitiza Waziri.

 

Ameongeza kuwa kuna miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo  yanayowahusu  vijana hivyo iko haja ya baraza hilo kubuni miradi hiyo ili kupata fursa za kujipatia mikopo ya kusaidia kuwawezesha vijana hao .

 

Waziri amefahamisha  kuwa baraza la vijana ni vyema likaandaa na kupanga mikakati maalumu na kufanya maonesho makubwa yatakayotangazwa na kuonyesha kazi zao ili kuleta tija. 

 

"Tutahakikisha kuwa tufanya kila linalowezekana kuhakikisha  Baraza linafanya vizuri ili kusonga  mbele ,"alifahamisha.

 

Aidha amelipongeza  baraza la vijana kwa kufanya Mkutano huo kwani  ni  jambo jema ambalo litasaidia kuleta ushirikiano wa pamoja katika  kujadili  na kudhibitisha taarifa za Vijana na badae kutoa maazimio.

 

Nae Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Salum  Issa Ameir amesema katika mkutano huo kuna wajumbe 75 ambapo 71 kati yao  ndio watakaopiga kura .

 

Amesema lengo la kuwa na vijana ni kuwasadia katika changamoto zao na kuzigeuza kuwa ni fursa kwa kuwaunganisha pamoja kupitia makundi mbalimbali.

 

Amefahamisha kuwa katika mkutano huo watafanya kazi mbili ikiwemo kudhibitisha  na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu vijana.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Khamisi  Abdalla  amesema Wizara imejipanga katika kuwaendeleza Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia miradi mbalimbali waliyoianzisha.

 

Amesema Serikali itajenga Vyuo vitano vya amali katika kila Mkoa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia elimu na kuwajengea uwezo.

 

Mwenyekiti Baraza  la Vijana ameomba wizara  kupatiwa posho kwa wenyeviti wa Wilaya wakati utaporuhusu angalau kujisaidia


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.