Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amewanasihi Waumini wa Kiislamu kutekeleza kwa vitendo, Mafunzo na Miongozo ya Uislamu ili kudhihirisha Hazina na Utukufu wa Dini hii.
Alhaj Othman ametoa nasaha hizo leo, mara tu baada ya Swala ya Ijumaa, alipojumuika na Waumini mbalimbali wa Kiislamu, katika Msikiti wa Mtoro, Ilala Jijini Dar es Salaam, Tanzania Bara.
Amekumbusha kuwa utekelezaji wa Miongozo na Mafunzo Mema ya Dini yakiwemo Malezi bora kwa watoto, ni katika mambo ya msingi katika ustawi wa jamii, hasa ambayo inathamini hazina na utajiri wa Dini ya Kiislamu.
“Malezi tuliyopewa katika Dini ni wajibu tuyapeleke kwa kizazi chetu kwani ndiyo ambayo yatapelekea kupatikana kwa Watoto wema, Viongozi wema, na hatimaye Jamii Njema ”, ameeleza Mheshimiwa Othman akibainisha pia kwamba miongoni mwa changamoto kubwa za sasa katika umma na kote ulimwenguni, ni pamoja na ukosefu wa khulka njema zitokanazo na Malezi Mema.
Akibainisha zaidi matatizo ya umma kwa sasa, Alhaj Othman amefahamisha kuwa Waislamu wamekuwa na tabia ya kujikunyata kwa kujiona duni, na hivyo kukiuka ule wajibu wa kujitolea katika harakati za Dini na Malezi, kwa dhana kuwa wao ni maskini, wakiamini kama kwamba wenye dhamana ya Uislamu ni Matajiri na wenye mali pekee, huku akisisitiza kwa kusema, "mali na uwezo ni amana na ni dhamana, na hivyo tukumbuke kwamba ipo siku vitatuponyoka".
Hivyo amesema Malezi, Tabia Njema na Kujitolea kwa hali na mali kwaajili ya Dini na Ustawi Bora wa Jamii ya Kiislamu ni Muhimu na Wajibu wa Kila Mmoja, ikizingatiwa kwamba, hap Duniani Waislamu ni Mithili ya Sabuni, ikichafuka yenyewe hukosekana au huwa vigumu kujitakasa.
Pamoja na kutanguliza shukuran kwasababu ya Dua Maalum, Mheshimiwa Othman amewashukuru Waumini na Uongozi wa hapo kwa juhudi zao ambazo zimepelekea, huo kuwa ni zaidi ya Msikiti, bali Taasisi Kamili.
Akitoa Khutba Mbili wakati wa Ibada hiyo, Khatiib Sheikh Faraj Farjala Abdallah, amewakumbusha Waumini wa Kiislam akisema Utukufu wa Mitume hauwezi kuundoka kwasababu ya Vifo vyao, kwani Daraja yao ni kubwa Mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba ni Wajibu wa Waislamu kuutukuza.
Amesema kwamba kwa Waislamu na kwa Mnasaba wa Msimu huu wa Kumkubuka zaidi Kipenzi cha Mwenyezi Mungu na Mbora wa Viumbe wote, Mtume Muhammad (S.A.W.) inawapasa kujipamba kwa tabia njema ili kuendeleza Utukufu wa Mitume wote (Rehma na Amani Ziwafikie).
Swala hiyo ambayo Imeongozwa na Sheikh Abdalla Mohammed Al-Mundhir, imefuatiwa na Dua Maalum ya Kumuombea Mheshimiwa Othman, Nchi na Taifa kwa Ujumla, ikiongozwa na Imam Mkuu wa Msikiti huo, Sheikh Abbas bin Ramadhan.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Septemba 22, 2023
No comments:
Post a Comment