Habari za Punde

Waziri Mhe.Kairuki Aipongeza Makumbusho ya Taifa kwa Kuwa Wabunifu katika Utendaji Kazi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa pili kushoto) akimsikiliza Mhifadhi Akiolojia, Makumbusho ya Taifa, Justine Nkunge alipofanya ziara ya kikazi katika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia utendaji kazi.Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) na wengine ni watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa.

Na Happiness Shayo – Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameipongeza Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) kwa kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuweza kuitunza nyumba ya utamaduni, kuwa na namna mbalimbali za maonesho na mikusanyo zaidi ya laki nne nchini.

Waziri Kairuki ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea eneo la Makumbusho ya Taifa  pamoja na Kijiji cha Makumbusho kwa lengo la kuangalia utendaji kazi wao.

“Tumefurahia kwa jinsi ambavyo Makumbusho ya Taifa wameweza kuitunza nyumba ya utamaduni na kuwa wabunifu kwa kuanzisha aina mbalimbali za maonesho na kuwa na mikusanyo zaidi ya laki  nchini” alisema Mhe. Kairuki

Sanjari na hayo, Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watendaji wa Taasisi hiyo kuendelea kuwa wabunifu ikizingatiwa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepitisha muundo mpya kwa ajili ya taasisi hiyo.

Aidha, Mhe. Kairuki ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuboresha maeneo mapya hasa kwenye eneo la utafiti na kuhakikisha kwamba nafasi muhimu za rasilimaliwatu zinajazwa akitolea mfano nafasi za Maafisa Utamaduni na Maafisa Utalii.

Amesema lengo la kuendelea na maboresho mbalimbali katika Makumbusho ya Taifa ni kuvutia watalii wengi zaidi wanaokuja nchini na kuwafanya waweze kurudi kwa mara nyingine.

“Tunaangalia ni namna gani tutaweza kuvutia watalii waje nchini na wakija wasije mara moja, ni nini kitakachomvutia mtalii aje mwakani pia ndio maana tunaendelea kufanya ubunifu zaidi kuona ni namna gani kuwa na maonesho mengi ya aina mbalimbali ya kielimu, kiutamaduni na kiutalii katika makumbusho yetu pamoja na malikale" alisema Waziri Kairuki.

Vilevile, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuangalia namna bora za kuboresha

malikale nchini na amewakaribisha watu binafsi kuanzisha makumbusho zao ili kuhakikisha mila, utamaduni na historia za Mtanzania zinatunzwa.

Ziara hiyo iliyolenga kuangalia uwajibikaji imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula (Mb) na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi pamoja na watendaji na watumishi wa Makumbusho ya Taifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (katikati) akimsikiliza Afisa TEHAMA wa Makumbusho ya Taifa, Mtaki Mahinda akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa za makumbusho zinavyowekwa kidijitali,  katika ziara ya kikazi kwenye Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam . Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) na wengine ni watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (katikati) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Wilbard Lema akitoa ufafanuzi kuhusu nyumba za asili za kabila la Wanyamwezi, zilizopo kwenye Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam . Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) na wengine ni watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa pili kushoto) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Wilbard Lema akitoa ufafanuzi kuhusu nyumba za asili za Pwani zilizopo kwenye Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) (kushoto)na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga (kulia) .
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa pili kulia mstari wa mbele) katika picha ya pamoja na watumishi wa Makumbusho ya Taifa mara baada ya ziara yake ya kutembelea Makumbusho hiyo na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) (wa tatu kulia mstari wa mbele), Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi (wa tatu kushoto mstari wa mbele) na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga (kulia) .


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.