Meneja wa kitengo cha magonjwa yasioambukiza Omar Mohammed Suleiman akijibu baadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari kuhusiana na ugonjwa huo wakati wa utoaji wa taarifa ya utafiti wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasioambukiza (NCDs steps survey) unaotarajiwa kuanza Septemba 09 katika kaya 540 za Unguja na Pemba ,hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBAR
Na Rahma Khamisi Maelezo 8/9/2023
Wizara ya Afya Zanzibar inatarajia kufanya Utafiti wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza(NCDs step servey ) kuanzia kesho Septemba 9 mwaka huu.
Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na utafiti huo huko Ofisini kwake Mnazimmoja Naibu Waziri wa Afya Hassan Khamis Hafidhi amesema utafiti huo utafanyika Tanzania Nzima ambapo kwa upande wa Zanzibar utaanza Rasmi Siku ya Jumamosi katika Shehia zilizochaguliwa kitaalamu.
Naibu Waziri alifahamisha kuwa kwa mujibu wa miongozo ya Kitaalamu ya kiutafiti jumla ya kaya 540 zitahojiwa Unguja na Pemba na kuwataka wananchi wa kaya hizo kutoa ushirikiano na kuwapatia tarifa sahihi wataalamu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kwa kusema kuwa miongoni mwao taarifa zotakazokusanywa katika utafiti huo ni pamoja na vichecheo vinavyopelekea maradhi hayo ikiwemo matumizi ya pombe,tumbaku, uzito wa mwili, kiwango cha kuushughulisha mwili na ulaji wa matunda na mbogamboga,hivyo aliwataka wanakaya husika kuwa wawazi ili kupatikana kwa taarifa na takwimu sahihi.
Amesema lengo la utafiti huo ni kutathmini hali ya afya juu ya viashiria hatarishi na mwenendo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini kufuatia kuongezeka kwa magonjwa hayo mwaka hadi mwaka.
“Maradhi haya yamekuwa tishio duniani kote ambapo kwa Zanzibar yanaongezeka mwaka hadi mwaka jambo ambalo linatia hofu tushirikiane katika mapambano dhidi ya maradhi haya “.alisisitiza Naibu huyo
Utafiti kama huo ulifanyika Zanzibar mwaka 2011 na Tanzania Bara ulifanyika 2012 ambapo Zanzibar ilikua Nchi ya kwanza kufanya utafiti huo katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment