Habari za Punde

Maendeleo Makubwa Ndani ya Kipindi cha Miaka Mitatu ya Uongozi Wake Yametokana na Kuimarika kwa Mifumo ya Kidijitali Inayodhibiti Matumizi na Fedha za Serikali

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuendelea kuzuia na kudhibiti uvujaji fedha holela maeneo yote ya vyanzo vya mapato nchini ili kuboresha maendeleo kwa maslahi mapana ya nchi.

Alisema, maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake yametokana na kuimarika kwa mifumo ya kidijitali inayodhibiti matumizi na fedha za Serikali kupotea kiholela kwa maeneo yote ya vyanzo vya mapato ikiwemo viwanja vya ndege, bandarini, halmashauri na maeneo mengine.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye Kongamano la maadhimisho ya miaka mitatu ya uongozi wake, ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, kipimo cha uongozi wake na maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar, ndani ya kipindi cha miaka mitatu ni kuimarika kwa Utawala bora wenye kufuata katiba ya nchi, Sheria, kanuni, kuwashirikisha watu na kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi mapana ya nchi na watu wake.

Rais Dk. Mwinyi alieleza, hali hiyo imeimarisha amani, utulivu na mshikamano wa Wazanzibari bila kujali tofati zao za kisiasa, dini na uhalisia wa maeneo wanayotoka katika kujenga maendeleo ya pamoja.

Dk. Mwinyi alieleza hali ya utulivu wa nchi ilivyo sasa imewavutia wawekezaji wengi waliowekeza mitaji mikubwa kwenye sekta ya utalii na uwekezaji.

“Wawekezaji wanajali zaidi amani ya nchi wanayotaka kuwekeza mitaji yao, sisi bahati nzuri nchi yetu inafuata taratibu, sera na sheria za kumlinda mwekezaji” Alifafanua Rais Dk. Mwinyi

Akizungumzia mafaniko ya utekelezaji wa sera ya Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Mwinyi alisema, kupitia Sekta tano za sera hiyo ambazo ni Utalii, Uvuvi na ufugaji, bandari, Mafuta na gasi pamoja na biashara kupitia usafiri wa majini.

Alisema, mafanikio makubwa yamepatikana na Zanzibar inaongoza kupokea ndege kubwa za kimataifa zinazoleta watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Alisema, Serikali inatekeleza miradi mikubwa pia wawekezaji wengi wanainufaisha Zanzibar kwa kuongeza soko la ajira kwa wazawa, kupitia maeneo mbalimbali ya Utalii, Uvuvi, Ufugaji, Ukulima wa mwani, bandari na biashara za majini baina ya bandari za Unguja na Pemba, Dar es Salaam, Tanga, Kilwa, Mombasa na Komoro, kwa kukuza biashara kubwa na ndogo, kukua kwa soko la bidhaa zinazozalishwa nchini na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi yenye tija kwa maslahi mapana ya nchi.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali imewekeza mitaji mikubwa kwaajili ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, kiasi cha shilingi billioni 31 na zaidi ya dola za kimarekani milioni 10 sawa na shilingi bilioni 25 kutoka kwa Mfuko wa Khalifa pamoja na kuboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara hao kufuatia ujenzi wa masosko ya kisasa ya Mwanakwerekwe, Mombasa, Jumbi na Chuini na maeneo mengine ya Zanzibar.

Akizungumzia kero za badari ya Malindi, kilio cha mfumko za bei za bidhaa, Rais Dk. Mwinyi alieleza serikali iloivyochukua hatua cha kuondosha changamoto hizo kwa kuruhusu sekta binafsi kuedesha badari hiyo sambamba na Serikali kuendea na ujezi wa bandari jumuishi ya Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja itakayokidhi haja kwa matumizi ya babdari za kisasa.

Hata, hivyo Raisi Dk. Mwinyi aliahidi kuongeza kasi zaidi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka miwili ijayo ili kukamilisha ahadi alizoziweka kwa Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed alisema Wazanzibari wanashuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar kwa kipindi kifupi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. Minyi.

Alisema, Dk. Mwinyi ametekeleza ahadi zake kwa vitendo kama alivyowaahidi wananchi wa Zanzibar wakati anaingia madarakani na mafaniko yaliopo sasa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa alisifu juhudi kubwa za maendeleo zilizofanywa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake ni za kupigiwa mfano hasa kwewnye kuimarika kwa huduma za jamii kwa sekta zote za Afya, Elimu, Makazi na Maji safi na salama.

Alisema ndani ya kipindi kifupi Mkoa wa Mjini Maghabiri unajivunia kwa ujenzi wa skuli mpya 14 zikiwemo nane za ghorofa na madarasa 164 yenye miundombinu na vifaa vya kisasa, wajasiriamali 1200 wamepatiwa mitaji, boti za uvuvi na kuwekewa mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwemo ujenzi wa masoko ya kisasa, vituo vya mabasi vya kisasa vya Mnazi Mmoja, Kijangwani na Malindi, matangi makubwa ya maji safi yenye ujazo wa lita zaidi ya milioni 130 ujenzi wa miundombinu ya kisasa zikiwemo barabara za za urefu wa kilomita 115 na bandari za kisasa.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.