Habari za Punde

Tanzania Kupokea Ndege Mpya ya Abiria Aina ya Boeng B737-9 MAX Oktoba 3, 2023 Jijini Dar es Salaamu

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarwa akifafanua jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari juu ya ujio wa ndege mpya mpya ya abiria aina ya Boeing B737- 9 MAX jijini Dar es Salaam.

Dar es salaam
Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737- 9 MAX inatarajiwa kuwasili nchini kesho oktoba 3 katika uwanja wa Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 1

Akizungumza jijini Dar es Salaam juu ya ujio wa ndege hiyo waziri wa uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema  hafla ya mapokezi ya ndege hiyo itaenda sambamba na uzinduzi wa ndege mbili za mafunzo aina ya Cessna 172S.

Alisema mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za makusudi za kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuanza kuinunulia ndege mpya na kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi. Hadi Septemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege 12.

"Ikumbukwe kuwa mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za makusudi kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuanza kuinunulia ndege mpya na kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi. Hadi Septemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege 12 ambazo zimeshawasili nchini" Alisema Prof. Mbarawa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuhahakikisha kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania inatoa huduma zenye kuhimili ushindani kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya kikanda na kimataifa. 

Prof. Mbarawa alibainisha kuwa Julai, 2021 Serikali iliingia mikataba na Kampuni ya Boeing ya Marekani ya ununuzi wa ndege nne mpya zenye teknolojia ya kisasa ambapo amebainisha kuwa Ndege hizo ni ndege mbili za abiria za masafa ya kati aina ya B737-9MAX zenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege moja ya abiria ya masafa marefu aina ya B787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na ndege moja kubwa ya mizigo aina ya Boeing B767300F yenye uwezo wa kubeba tani 54. 

Alisema Ndege ya mizigo aina ya B767-300F tayari ilishawasili na inaendelea kutoa huduma zake na ndege moja ya masafa ya kati aina ya B737-9Max uundaji wake umekamilika na inatarajia kuwasili nchini kesho Oktoba 3, 2023 na Ndege mbili zinaendelea kuundwa ambapo zinatarajia kuwasili nchini  Disemba, 2023 na Machi, 2024.

"Ndege ya abiria ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX ambayo uundaji wake umekamilika inatarajia kuwasili nchini tarehe 03 Oktoba, 2023. Ndege hiyo inauwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo daraja la kawaida “economy class” ni abiria 165 na daraja la biashara (business class) abiria 16, pia uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa masaa 8 bila kutua," Alisema Prof. Mbarawa.

Aidha Prof. Mbarawa aliongeza kuwa Kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 13 mpya zilizonunuliwa kutokana na utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na hivyo kuwa na ndege 14 zinazosimamiwa na ATCL katika uimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari zake ndege kwa  soko la  ndani, kikanda na kimataifa.  

Alisema hatua hizo ni pamoja na kukijengea uwezo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kukijengea majengo, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia, ununuzi wa ndege  za mafunzo, na kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili kutoa Kozi za muda mrefu za Uhandisi wa  Matengenezo ya Ndege  (Degree and Diploma); Kozi za  kutoa mafunzo ya Wahudumu wa Ndani ya Ndege (Cabin Crew) na Uendeshaji wa Safari za Ndege; Pamoja na Ndaki ya Chuo cha Urubani (Flight Crew).
 
"Hadi sasa Chuo kinatoa mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, Uendeshaji wa Safari za Ndege pamoja na Uhudumu wa Ndani ya Ndege kwa Ithibati za TCAA. Vilevile, Chuo kinatoa mafunzo ya Air Fares and Ticketing, Airport Operations Fundamentals, Airline Marketing pamoja na Airline Customer Service kwa Ithibati ya IATA," Alisema Prof. Mbarawa.

Alisema Katika kuongeza ufanisi wa mafunzo ya urubani Juni, 2023 Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha NIT kuingia mkataba na ununuzi wa ndege  moja ya mafunzo ya injini mbili aina ya Beechcraft Baron G58 toka Kampuni ya Textron Aviation Inc. ya Marekani na Ndege hiyo inatarajia kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kuwasili kwa ndege hii kutawezesha wahitimu wa kozi ya CPL kufanya mafunzo ya Multi-Engine Class Rating na Multi-Engine Instrument Rating hivyo kukidhi vigezo vya kuingia kwenye ajira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.