Habari za Punde

Zanzibar yajipanga kufanya mabadiliko sekta ya ElimuWaziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela  Mohammed  Mussa Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na mageuzi katika sekta ya elimu huko Ofisini kwake Mazizini Mjinin Unguja.

 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inakusudia kufanya mabadiliko ya mfumo wa Elimu ya Amali kuwa Elimu ya lazima baada ya kukamilika marekebisho ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1982 na Sera ya Mwaka 2006.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Mazizini Unguja, juu ya mabadiliko ya Elimu ambayo yanatarajiwa kufanyika.

Amesema  hatua hiyo inakuja kufuatia mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Maandalizi na Msingi ulioanza kutumika Mwaka huu wa 2023.

Amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuwawezesha wanafunzi watakao maliza darasa la kumi kuendelea na Elimu yao katika madarasa ya Elimu ya Amali jambo ambalo litawasaidia kuwa na ujuzi na maarifa watakapomaliza masomo yao

Aidha,amesema kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itafuta mitihani ya Taifa ya darasa la Nne na Kumi baada ya kuona  matokeo mazuri ya utekelezaji wa Mtaala mpya wa ujenzi wa umahiri.

Sambamba na hayo, amesema, Wizara imekuwa na mikakati ya kuona wanafunzi wanaingia katika mkondo mmoja ambapo mpango huo unaendelea na Kwa baadhi ya Skuli wameshaanza kuingia mkupuo mmoja.

Akizungumza mfumo wa Elimu, amesema mfumo uliokuwepo wa mwaka 2016 utaendelea kuwepo kama ulivyo na watarudi kwenye sera kuona namna gani ya kuisimamia Sera ambapo kwa Sasa wamerudi katika darasa la Saba kupitia Sera hiyo iliyokuwepo awali.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).

Tarehe:18/10/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.