Habari za Punde

KONGAMANO LA TANO LA WAFANYAKAZI WA HUDUMA ZA TIBA ZA DHARURA WAFANYIKA ZANZIBAR

Makamu wa pili wa Rais akipokea zawadi maalum kwa niaba ya Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi kutoka kwa rais wa chama cha wafanyakazi wa huduma za  tiba za dharura  EMAT dkt. Juma Mfinanga katika mkutano wa  tano wa wataalamu wa tiba za dharura huko Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Na Fauzia Mussa,     Maelezo Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazurui amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti juu ya namna ya kukabiliana na majanga ya ajali, dharura na maradhi yasiyoambukiza ili kupunguza ulemavu na vifo vitokanavyo na maradhi hayo.

Akizungumza katika mkutano wa   tano wa  huduma za tiba za dharura Tanzania, huko Goleden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar Waziri huyo alisema  Serikali zote mbili zinaendelea kuimarisha huduma za Dharura  kwa kuweka miundombinu madhubuti ikiwemo vifaa tiba vilivyofungwa katika maeneo tofauti ya kutolea huduma hizo Tanzania bara na visiwani.

Alifahamisha kuwa Serikali hizo zina lengo la kuendeleza huduma za dharura kwenye ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya kuanzia kwenye ngazi ya jamii hadi rufaa kwa lengo la kutimiza lengo la huduma za Afya zenye usawa kwa wote pamoja na kuahidi kusimamia ipasavyo vitengo hivyo ili kutoa huduma zenye  viwango.

Alisema katika  kupunguza changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa na bobezi katika vitengo vya dharura, Wizara ya Afya imeiweka fani hiyo katika vipaombele vyake, na kuwataka Wanafunzi wanaomaliza masomo ya Sekondari  kusomea kada hiyo ili kuongeza wataalamu watakaosaidia kuongeza chachu ya upatikanaji wa huduma bora na endelevu za tiba za dharura Nchi nzima.

“Tafiti zinaonesha kuwa kila kwenye watu laki moja (100,000) kunapendekezwa kuwe na wataalamu wa tiba za dharura kumi na tano (15) kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi wa eneo husika ili kupunguza magonjwa mbalimbali na vifo vinavyoweza kuepukika, kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2022, Watanzania tupo takriban bilioni 60 na Zanzibari karibu ya milioni mbili (1,889,773), takwimu hizi zinaonesha uhitaji mkubwa wa wataalamu bingwa wa tiba za dharura nchini.”Alifafanua Waziri huyo.

Alisema Kongamano hilo lililojadili  namna ya uwekaji wa mifumo imara ya utoaji wa  huduma za Afya za dharura, kuimarisha afya ya jamii na kuzifanya kuwa  endelevu limefanyika  wakati muafaka ambapo Serikali zote mbili zimeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha huduma hizo.

Awali Waziri Mazrui alimshukuru   Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa  kuipa kipaombele kada hiyo pamoja nakuwashukuru Wanachama wa huduma za Tiba za Dharura EMAT kwa kushirikaiana na Wizara ya Afya kuandaa kongamano hilo lililokwenda sambamba mabadiliko ya sera ya Afya kwa kitita cha huduma za Afya nchini.

Kwa upande wake Rais wa chama cha wafanyakazi wa huduma za tiba za dharura (EMAT) Dkt. Juma Mfinanga alisema wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakuwa na madaktari wenye taaluma katika kitengo cha huduma za tiba za dharura ili kuhakikisha vifo vinavyotokana na majanga vinapungua Nchini.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi na kuwashirikisha wadau tofauti kwa lengo la  kubadilishana uzoefu na taaluma ili kuharakisha ukuaji wa huduma za dharura nchinini,  kupunguza vifo vya mama na watoto, vifo vitokananvyo na maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza na vifo vinavyotokana na ajali na majanga mbali mbali. 

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazrui akizungumza katika  Mkutano wa tano wa huduma za tiba  za dharura huko Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.


Baadhi ya wadau wa huduma za  tiba za dharura wakiwa katika mkutano wa tano wa huduma za tiba za dharura huko Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.