Habari za Punde

Wananchi Waliopangishwa Nyumba Zinazosimamiwa na Shirika la Nyumba Zanzibar Kuzingatia na Kufuata Sheria na Taratibu Zilizowekwa

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali akizungumza na wapangaji wa nyumba za Mombasa kwa Mchina kupitia kikao maalum kilichoandaliwa na Shirika la Nyumba Zanzibar ambapo amewataka wapangaji hao kuzingatia sheria na taratibu.


Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Mkaazi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali amewataka wananchi waliopangishwa katika nyumba zinazosimamiwa na shirika la Nyumba Zanzibar kuzingatia na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili nyumba hizo ziendelee kutumiwa na vizazi vijavyo.

Mhe. Waziri Rahma Kassim Ali ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi na wakaazi wa nyumba za Mombasa kwa mchina kupitia kikao maalum kilichoandaliwa na uongozi wa Shirika la nyumba Zanzibar.

Mhe. Waziri amesema nyumba hizo zina masharti na miongozo yake ambayo imeanishwa katika mikataba hivyo, kila mmoja anatakaiwa kuzingatia masharti hayo ili kuepuka kwenda kinyume na maelekezo ya Shirika la Nyumba.

Waziri Rahma amefafanua kuwa, miongoni mwa mambo yasioruhusiwa katika nyumba hizo ni pamoja na kuzungusha maturubali au kuzungusha makuti katika nyumba hizo, kufungua gereji  pamoja na kufungua sehemu za kuoshea magari.

Katika hali hiyo Mhe. Waziri ameuomba uongozi wa Wilaya kupitia Mhe. Mstahiki Meya kuchukua hatua kwa watu waliobadilisha matumizi ya maeneo hayo kwa kufanya kazi zisizoruhusiwa ikiwemo kufungua maegesho kwa ajili kuuza magari (Showroom).

Aidha, Mhe. Rahma amewakumbusha wananchi kuendelea kuvithamini na kuvitunza vitu vya Serikali kwani siku zote vitu hivyo vimekuwa vikiwahudumia watu wengi kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar Ndugu Mwanaisha Ali Said amewakumbusha wapangaji wa nyumba hizo juu ya suala zima la ulipaji wa kodi kwani kufanya hivyo kutalisaidia Shirika kuweza kufanya ukarabati wa nyumba kwa wakati.

Mkurugenzi Mwanaisha amewaomba wapangaji hao kutoa kipau mbele maalum kwa kufaya usafi katika maeneo yaliowazunguka badala ya kusubiria kazi hiyo kufanywa na Shirika.

“Niwaombe sana wapangaji wetu munapaswa kuzingatia suala la usafi kwani jukumu hilo sio la Shirika pekee yake tunapaswa kushirikiana katika jambo hili” Alisema Mkurugenzi Mwanaisha

Pia, Mkurugenzi ametoa katazo kwa wapangaji wa nyumba hizo kutopaka rangi kila mtu aina anayoipenda bila ya kupata maelekezo maalum kutoka kwa uongozi wa Shirika kwani nyumba hizo zinatakiwa ziwe katika muonekano wa aina moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya Makaazin Hannat Bakar Hamad ametoa wito kwa wananchi kujitokeza na  kuunda Jumuiya na kufanya usajili kwa lengo la kuweza kutatua changamoto za makaazi zinazowakabili wananchi.

Amesema uwepo wa Jumuiya hizo kwa namna moja au nyengine kutasaidia uanzishwaji wa sheria na kanuni ndogo ndogo zikazowezesha kuweka usalama wana watu na makaazi yao.

Wakitoa maoni yao, wapangaji wa nyumba hizo wamesema katika siku za karibuni kumekuwa na uvamizi mkubwa wa watu katika maeneo hayo kwa kufanya kazi zisizoruhusiwa jambo ambalo linapelekea baadhi ya wakaazi wa eneo hilo kujenga hofu hasa kwa watoto wao.

Wameuomba uongozi wa Shirika la Nyumba kuchukua hatua za maksudi ya kulipatia ufumbuzi suala la kutuama kwa maji taka katika eneo hilo na wao wapo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika.

Baada ya kikao hicho, Mhe. Waziri alipata fursa ya kutembelea na kukagua maenedeleo ya ujenzi wa Nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba zilizopo Mombasa kwa Mchina.

Mapema asbhi, Mhe.Waziri alifanya ziara katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuskiliza na kuipatia ufumbuzi  migogogro mbali mbali inayohusiana na masuala ya ardhi.

Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Makaazi Ndugu Hannat Bakar Hamad akiwasisitiza wananchi na wapangaji wa nyumba za Mombasa kuunda Jumuiya maalum na kuzisajili ili kuimarisha hali ya usalama wao na makaazi yao
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar Ngugu Mwanaisha Ali Said akiwakumbusha wapangaji wa nyumba za Mombasa kwa Mchina kulipa kodi kwa wakati kupitia kikao maalum kilichondaliwa na Shirika hilo kilichofanyika humo Mombasa kwa mchina.

Wapangaji wa nyumba za Momba kwa Mchina wakitoa maoni yao kupitia kikao maalum kilichoandaliwa na uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar ambapo wameuomba uongozi kuipatia ufungumbuzi changamoto ya kutuama kwa maji taka katika makaazi yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.