Habari za Punde

DKT MPANGO AFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA MADAKTARI WA MOYO AFRIKA

 Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Asha Ressa Izina akimkabidhi zawadi maalum Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango katika mkutano wa kimataifa wa madaktari bingwa wa moyo Afrika  uliofanyika Hoteli ya Golden tulip uwanja wa ndege Zanzibar

Na Fauzia Mussa Maelezo Zanzibar

Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango amesema Serikali imejipanga kuendelea kuwekeza katika hospitali   ili kuhakikisha Tanzania inaenda sambamba na mabadiliko ya huduma za afya.

Akifungua mkutano wa madaktari bingwa wa moyo Afrika  uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip amesema mpango huo umezingatia zaidi kuwa na vifaa vya kisasa pamoja na kusomesha madaktari wake kwa idadi kubwa ili kutosheleza katika kuwafikia wananchi.

Amesema Serikali imeona ipo haja ya  kuimarisha taasisi kama hizo pamoja na hospitali zake nchi nzima  ili kupunguza athari zaidi zitokanazo na magonjwa kama hayo.

Amesema magonjwa ya moyo yamekuwa yakiongezeka na kuchangia vifo vingi siku hadi siku hivyo hivyo aliwataka wananchi na madaktari kuyatumia vyema mafunzo hayo ili kujikinga na kujitibu pale wanapopata magonjwa hayo.

Nae Waziri wa afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ummi Ali Mwalim amesema Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 9 kuwasomesha madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa ya moyo ili kuimarisha huduma za matibabu nchini.

“Tunataka kuona tunafikia hatua ya kuwa wagonjwa kutoka nje ya Tanzania wanatibiwa nchini kwetu, na madaktari wetu wanatoka kuongeza nguvu za matibabu nchi jirani”, alisema waziri Ummy

Alieleza kuwa lengo la wizara ni kuwa na hospital kubwa ya magonjwa ya moyo Daer-es-salaam na kuwa na matawi katika mikoa mengine ikiwemo Arusha ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu bora Afrika Mashariki.

 Kwa upande wake Naibu Waziri wa afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amehimiza wananchi kujikinga na magonwa hayo kwa kufuata ushauri wa madaktari ikiwemo kuwa na utamaduni wa kufanya mazowezi.

Amesema Tanzania ni nchi  inayokabiliwa na changamoto ya maradhi yasioambukiza ikiwemo saratani na magonjwa ya moyo hivyo amewataka

 wananchi kubadili mtindo wa maisha kwa  kula mlo sahihi na  kuacha matumizi ya pombe kupita kiasi  ili kuepuka magonjwa ya moyo na figo ambayo yamekuwa na gharama kubwa katika matibabu yake.

 “Umefika wakati sasa wa kufanya bidii ya kujilinda na magonjwa haya, kati ya vifo 5 vinanvyotokezea  hospitali ya mnazimmoja vinne au vitatu kati ya vifo hivyo  ni vya maradhi yasioambukiza” alisema  naibu waziri

 

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Richard Kisenge amesema ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo umepelekea serikali kuanzisha taasisi hiyo ambayo ni mfano kwa afrika mashariki katika kutoa huduma bora .

Amesema Taasisi hiyo ina mpango wakuwafundisha wananchi na watendaji wa chini ili kuweza kumhudumia mgonjwa mara tu anapopata mshtuko wa ghafla  wa moyo au sindikizo la juu la damu ili kupunguza athari zaidi.

Amesema takribani watu 300 wanapokelewa katika taasisi hiyo kwa mwaka ambapo asilimia zaidi ya 15 kati yao wanasumbuliwa na sindikizo la damu lililopelekea mioyo yao kutanuka.

Alifahamisha kuwa zaidi ya watu milioni 17.9 Duniani hupata  magonjwa ya moyo  na robo ya wagonjwa hao hufariki kwa kila mwaka .

Katika mkutano  huo ulioandaliwa na JKCI zaidi ya wataalamu mia tano wa afya  kutoka mataifa mbali mbalimbali wameshiriki na  mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo  namna ya kujikinga na ugonjwa wa moyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.