Na Fauzia Mussa-Maelezo Zanzibar
Afisa wa afya ya jamii wizara ya afya Mwinyi Khamis amesema licha ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kupambana na ugonjwa wa malaria bado jamii haipo tayari kuunga mkono juhudi hizo jambo ambalo linapelekea kuongezeka kwa ugonjwa huo visiwani Zanzibar.
Akizungumzia hali ya malaria nchini katika mafunzo ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya mripuko yakiwemo malaria, macho na matumbo huko kitengo cha elimu ya afya Sogea amesema takwimu za wizara ya afya zinaonyesha kuwa ugonjwa huo umeongezeka takribani kwa wilaya zote za Zanzibar na kuwaathiri zaidi wanaume wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45.
“wanaoathirika zaidi kwa ugonjwa huu ni wanaume ikiwemo waendesha boda boda, wajenzi wa usiku, wanakwenda kumbi za starehe usiku pamoja na watazamaji mpira nyakati za usiku”, alifahamisha.
Alieleza kuwa kutokana na takwimu hizo wilaya ya mjini inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ikifuatiwa na wilaya ya magharibi B.
Amesema hali ya ongezeko la ugonjwa huo ni kutokana na jamii kutokutumia njia za kujikinga ikiwemo kulala kwenye vyandarua ,kuchelewa kufika vituo vya afya kwa wenye dalili za ugonjwa , kuwepo kwa mazalia ya mbu pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha amesema wizara kupitia kitengo cha elimu ya afya inaendelea kudhibiti ugonjwa wa malaria kwa kutoa elimu ya afya kwa jamii, tiba kwa wale waliogundulika kuwa na vimelea vya malaria, upigaji wa dawa majumbani kwa maeneo yaliathiriwa zaidi, kutoa dawa na kuichunguza damu jamii iliyo karibu na mgonjwa, pamoja na kutia viatilifu kwenye madimbwi ya maji.
Akizungumzia hali ya macho mekundu, Mratibu wa huduma za Afya ya Msingi na matibabu ya macho Dkt Rajab Mohammed Hilal amesema jumla ya watu 12860 wamepatiwa matibabu katika vituo mbalimbali vya afya Zanzibar na kwa sasa hali ya ugonjwa huo imepungua.
Mratibu huyo aliisisitiza jamii kuacha utamaduni wa kutumia dawa za kienyeji na kufika katika vituo vya afya ili kupata matibabu sahihi.
“Baadhi ya takwimu kwa wagonjwa waliotibiwa katika vituo vyetu kwa Zanzibar ni pamoja na wagonjwa 1,459 katika kitengo cha matibabu ya macho Hospitali ya Mnazi mmoja, 3,432 Kwamtipura, 2,316 Mpendae, 22 Chake chake,1,320 Kivunge, 993 Wete,25 Shungi, Kambini kichokochwe 65, 54 Wesha, 65Wingwi, 100 Pujini, 480 Micheweni ,na 660 Mkoani .” alieleza mratibu huyo
Akiwasilisha mada ya mazingira Meneja wa Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar Bakari Hamad Magarawa amesema hali ya uchafu wa mazingira inachangia ongezeko la magonjwa ya mripuko ikiwemo malaria na kipindupindu na kuitaka jamii kudumisha usafi katika maeneo yao pamoja na kuzingatia maelezo ya kitaalamu ili kujiepusha na magonjwa hayo.
Jumla ya watu 11 wamefariki kutokana na ugonjwa wa maleria kuanzia Januari 1 hadi januari 26 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment