Habari za Punde

Taasisi za Fedha Zakopesha Trilioni 33

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)

Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesema kuwa hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2023, mikopo yenye jumla ya shilingi trilioni 33.2 imetolewa na Benki na taasisi za fedha ambazo hutoa mikopo yenye dhamana inayotosheleza (fully secured), yenye dhamana inayotosheleza sehemu tu ya mkopo(partially secured) na isiyo na dhamana (unsecured).

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Shally Josepha Raymond, aliyetaka kujua ni kiasi gani cha mikopo na mitaji imetolewa na Taasisi za Fedha kwa wananchi kwa dhamana ya mali zilizorasimishwa na Wanawake wangapi wamenufaika.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa kwa sasa Serikali haina takwimu zinazotenganisha mikopo iliyotolewa kwa wanaume na wanawake, hata hivyo Benki Kuu ya Tanzania inatengeneza mfumo ambao ukikamilika utaweza kukusanya takwimu zinazotenganisha mikopo iliyotolewa kwa wanaume na wanawake kutoka kwenye benki na taasisi za fedha.

‘‘Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa sheria ya miamala salama na masjala bayana ya kielektroniki itakayotumika kusajili dhamana zinazohamishika ili kupanua wigo wa dhamana na hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata mikopo kutoka benki na taasisi za fedha, ’’alifafanua Dkt. Nchemba.

Vile vile, Mhe. Dkt Nchemba alijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaweka kituo kidogo cha forodha katika Kata ya Itiryo/Bikonge pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kupata bidhaa kutoka Kenya.

Akijibu swali hilo Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa kituo cha forodha Kata ya Itiryo/Bikonge ni miongoni mwa vituo tarajiwa vya forodha vitakavyofanyiwa tathmini na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mwaka wa fedha 2024/25.

‘‘Tathmini itafanyika kwa kuzingatia vigezo mahsusi ikiwemo uwiano wa gharama za ukusanyaji mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa katika kituo hicho. Endapo kituo hicho kitakidhi vigezo, mchakato wa uanzishaji wake utaanza kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,’’alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba aliwasisitiza wafanyabiashara wanaotumia mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Kata ya Itiryo/Bikonge, kuendelea kutumia vituo rasmi vya forodha vya karibu ikiwemo Kituo cha Forodha cha Sirari ili kurahisisha zoezi la ulipaji kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.