Habari za Punde

Waandishi Wameshauriwa Kuandika Habari za Mchezo na jinsia ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii


Na Fauzia Mussa. Maelezo. 14.05.2024.

Waandishi wa Habari nchini wameshauriwa kuandika habari  za michezo na jinsia ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii juu ya dhana ya michezo na jinsia.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (Tamwa) ofisi ya Zanzibar Dkt. Mzuri Issa wakati alipokuwa akizungumza na jopo la  Waandishi wa habari  za jinsia na michezo huko Tunguu Mkoa wa kusini Unguja.

Amesema masuala ya michezo kwa wanawake yamekuwa hayazungumzwi ipasavyo jambo ambalo linapelekea kukosa fursa mbalimbali zinazotokana na michezo ikiwemo afya, ajira na kipato.

Aidha amewataka Wananchi kuachana na dhana potofu ya kuwa, Wanawake kushiriki katika michezo ni uhuni jambo ambalo halina ukweli ndani yake.
Hata hivyo aliwataka waandishi hao, kuutumia ipasavyo mradi wa maendeleo ya Michezo Afrika ili kuleta mabadiliko katika jamii na kufikia hatua ya  wanawake na wasichana kuweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya michezo.

Sambamba na hayo amewataka kufuatilia na kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Muwezeshaji wa mafunzo hayo Bi Hawra Shamte amesema usawa wa kijinsia unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mila na tamaduni, ubaguzi wa kisheria, ukosefu wa elimu, fikra na dhana potofu ya kijinsia, uchumi na ajira mambo ambayo yanakwamisha wanawake kushiriki katika michezo.

Amesema wanawake wanahaki ya kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa kikapu, ngumi na  mpira wa miguu pekee bila kuathiri Mila,desturi na tamaduni zao.

Hivyo jamii , pamoja na wadau wanapaswa kuunga mkono michezo Kwa kuzingatia jinsia  ili  wanawake na wao  waweze kupoga hatua za maendeleo kupitia michezo.
“Tofauti za kimaumbile zinaonekana kikwazo katika michezo ingawaje kuna baadhi ya wanawake wanafanya vizuri zaidi kuliko wanaume katika michezo, umefika wakati sasa WA Wanawake kushiriki michezo Kwa maendeleo.” mwezeshaji  huyo.

Nao baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki katika mafunzo hayo wameahidi  kuyafanyia kazi na kuleta mabadiliko katika jamii juu ya suala zima la ushiriki wa Wanawake katika michezo na maendeleo.

Mradi wa maendeleo ya Michezo Afrika "SPORTS DEVELOPMENT AFRICA, EMPOWERING GIRLS THROUGH SPORTS IN ZANZIBAR” una lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia michezo unaendeshwa  Kwa mashirikiano kati ya  TAMWA ZNZ, Chama cha wanasheria wanawake (ZAFELA), chini ya ufadhili wa shirika la michezo la Ujerumani (GIZ).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.