Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Afunga Kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kwahani kwa Tiketi ya CCM Ndg. Khamkis Pele

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akimnadi na Kumkabidhi Ilani ya Chama Hicho Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kwahani kupitia Tiketi ya CCM Ndugu, Khamis Yussuf Mussa (PELE) katika Ufungaji wa kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo hilo zilizofanyika katika Viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti Zanzibar.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Chama cha Mapinduzi kiko imara na kitaendelea kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa Jimbo la Kwahani na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020-2025 kutokana na kuitekeleza vyema Ilani ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Akimnadi Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kwahani kupitia tiketi ya  CCM Ndg Khamis Yussuf Mussa Pele wakati wa kufunga kampeni za jimbo hilo katika viwanja vya kibanda maiti , Mhe. Hemed amewataka wananchi wa Jimbo la kwahani kumpigia kura za ndio mgombea huyo ili aendeleze kuinadi na  kitekeleza vyema ilani ya CCM.

Amesema endapo wananchi wa jimbo la Kwahani hawatafanya makosa na watamchagua ndugu Pele kuwa mbunge wa jimbo hilo ambae atashirikiana na wabunge na viongozi wengine katika kuitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi hasa katika kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo.

Mhe. Hemed amewataka wana CCM wa jimbo la kwahani kudumisha amani na utulivu wakati wote wa zoezi la uchaguzi na kuwasihi watakapomaliza kupiga kura kuŕudi majumbani kusubiri matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi.

Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib amesema wana CCM wa jimbo la kwahani wanaahidi kumchagua kwa kishindo ndugu Khamis Pele ambae anatosha kuwa Mbunge kutokana na uchapa kazi wake katika chama, uaminifu na kujitoa kwake katika kuitumikia CCM vinatosha kuipeperusha bendera ya CCM katika Bunge.

Talib ametoa onyo kali kwa wale wote wanaotumia majukwaa kwa kuwatukana na kuwakashifu Viongozi wakuu wa nchii na kusema kuwa CCM haitakuwa tayari kuvumilia uovu huo na itaviomba vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa maslahi ya Taifa.

Akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa  Mbunge wa Jimbo la Kwahani ndugu Kahamis Yussuf Pele ameahidi ataitekeleza vyema Ilani ya CCM kwa kukaa pamoja na viongozi wengine wa Jimbo kupanga mikakati ya kimaendeleo ili  kuweza kuleta Ustawi ndani ya Jimbo hilo la kwahani.

Pele amewashukuru Viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa imani kubwa waliyompa ya kumteuwa kuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kwahani ambapo amesema kazi yake kubwa ni kuhakikisha anayatekeleza kwa vitendo yale yote yaliyoelezwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.