Habari za Punde

FAINALI ZA JIMBO CUP RUANGWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi kikombe Nahodha wa Kikosi cha Kiwengwa FC Yahaya Abdallah Khamis, katika fainali za Jimbo Cup, zilizofanyika kwenye uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Mkoani Lindi, ambapo Kiwengwa FC ilishinda kwa penati goli 4-1 dhidi ya Stand FC.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja Kikosi cha Kiwengwa FC ambao ni mabingwa wa Jimbo Cup 2024, kwenye fainali zilizofanyika kwenye uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Mkoani Lindi, ambapo Kiwengwa FC iliibuka mshindi kwa penati ya goli 4-1 dhidi ya Stand FC.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, katika fainali za Jimbo Cup, zilizofanyika kwenye uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Mkoani Lindi, ambapo Kiwengwa FC ilishinda kwa penati goli 4-1 dhidi ya Stand FC, Novemba 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa ameshuhudia mchezo wa fainali ya kombe la jimbo maarufu Jimbo cup kati ya Stand fc na Kiwengwa FC uliofanyika katika uwanja wa mpira wa miguu wa Majaliwa, Ruangwa Mkoani Lindi.


Katika mchezo huo uliopigwa Novemba 25, 2024, timu ya kiwengwa Fc iliibuka bingwa baada ya kuwatandika Stand Fc kwa mikwaju ya Penati 4-1.


Akizungumza baada ya mchezo huo Mheshimiwa Majaliwa amesema michezo hiyo inatumika kuboresha maendeleo ya mpira wa miguu katika wilaya hiyo.

 

“Nitazungumza na chama cha makocha Taifa ili watupatie wakufunzi ambao watakuja kuwapa mafunzo makocha wa wilaya ya Ruangwa ya namna bora ya kusimamia timu zetu”

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa kuwa Wilaya ya Ruangwa imeamua kujidhatiti kwenye mpira wa miguu ni muhimu kuwa na waamuzi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia michezo “Chama cha Mpira cha Wilaya orodhesheni marefa waliopo katika wilaya hii, nitaomba uongozi wa marefa tupate kiongozi mmoja ili aje aendeshe semina kwa marefa wetu”

 

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kupitia michezo hiyo itasaidia kuongeza nguvu kwenye timu ya Namungo inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara “Chama cha Mpira kimechagua wachezaji 18 kupitia michezo hii, nataka nimuagize mwenyekiti, wachezaji hawa waingie kambini mapema”

 

Mshindi wa kwanza wa michezo hiyo amejipatia Shilingi milioni tano, jezi seti mbili, mipira miwili pamoja na kombe. Mshindi wa pili amepata shilingi milioni nne, mpira mmoja pamoja na jezi seti mbili.

 

 Michuano hiyo ilibeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 kupitia kauli mbiu yake "Piga Mpira Piga Kura, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Jambo letu sote"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.