Habari za Punde

Jumuiya ya RAWWAZA Yakabidhi Vifaa vya Usafi Kituo cha Afya Kibondeni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja

Na Takdir Ali. Maelezo.01.11.2024.

Watu wenye uwezo na Wafadhili  wameshauriwa kuelekeza zaidi nguvu zao katika miradi ya  jamii ili iweze kuwasaidia Wananchi.

Hayo yameelezwa na Daktari Dhamana wa kituo cha Afya Fuoni Kibondeni Dkt. Seif Ali Haji wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kupokea msaada wa vifaa vya usafi kutoka Jumuiya rafiki wa Wanawake na Watoto Zanzibar (RAWWAZA).

Amesema kukabidhiwa kwa vifaa hivyo ni kuonyesha jinsi Jumuiya ya RAWWAZA inavyoshirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusukuma mbele gurudumu la afya bora kwa Mwananchi.

Aidha amesema Serkali imekuwa mstari wa mbele katika kutoa vifaa mbalimbali ikiwemo vya usafi lakini mahitaji ni makubwa hivyo vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zilizopo.

Aidha na hayo amesema bila ya kuwepo vifaa vya usafi katika kituo cha Afya hawawezi kutoa huduma bora kwa jamii hivyo amewaomba wananchi kuiga mfano wa Jumuiya rafiki wa Wanawake na Watoto katika kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuwahudumia Wananchi wake.

Kwa upande wake Mjumbe wa Jumuiya Rafiki wa Wanawake na Watoto (RAWWAZA) Farashuu Mussa Abdallah na Balozi Mkuu wa Jumuiya hiyo Mwanakhamis Mselem wamesema lengo la kukabidhi vifaa hivyo ni kuunga mkono Serikali ya awamu ya nane, inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuwapatia afya bora Wananchi.

aidha wamesema baadhi ya vituo vya afya vinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya vituo vya Afya hivyo wameamua kukabidhi vifaa hivyo ni kuunga mkono mikakati iliowekwa na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake ikiwemo upungufu wa vifaa vya kufanyia usafi.

Jumuiya Rafiki wa Wanawake na Watoto Zanzibar (RAWWAZA) imekabidhi vifaa mbalimbali vya usafi katika Kituo cha Afya Fuoni Kibondeni ikiwemo Sabuni na Mashuka ya kulalia ili kuweza kuwasaidia Wananchi wanaotumia kituo hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.