Habari za Punde

Uhusiano wa Asili Kati ya Tanzania na Hispania Kuongeza Fursa Nyingi za Maendeleo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Othman Masoud Othman, amesema Uhusiano wa tangu asili, kati ya Tanzania na Hispania unaweza kuongeza fursa nyingi za maendeleo, baina ya Nchi Mbili hizo, zikiwemo za Kukuza Afya ya Jamii. 

Mhe.Othman ameyasema hayo Novemba 18, 2024 akizungumza na Madaktari Bingwa na Wataalamu, alipotembelea Hospitali ya 'De Clinica CEMTRO', Mjini Madrid, Nchini Hispania.

Amesema uhusiano huo wa tangu asili unahitaji kuendelezwa kwa lengo la kusaidia uimarishaji wa kutoa huduma bora za jamii, ili kufanikisha pia azma ya kujiletea maendeleo ya kweli.

Amefahamisha kuwa pindipo Azma ya Kuwaleta Madaktari Bingwa kuja Nchini, kwa lengo la Kuimarisha Afya ya Jamii na Huduma za Upasuaji itatekelezwa, kama ambavyo imeahidiwa kupitia Ziara hiyo, basi uhusiano kati ya Hispania na Zanzibar, Nchi ambazo zina Historia kubwa na mashirikiano ya muda mrefu, utazidi kuleta tija na mafanikio.

Amesema Serikali ya Zanzibar imepokea vyema na kwa mikono miwili, Ahadi ya Msaada wa Vifaa Tiba, na Madaktari Bingwa wakiwemo wa Mifupa, Magonjwa ya Watoto, na  Akinamama, ambao wameahidi Kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kutoka Hospitali hiyo, kwa Lengo pia la kuwaongezea ujuzi, Wataalamu wa hapa Nchini.

Akitoa ahadi hiyo, Muanzilishi wa Hospitali ya De Clinica CEMTRO, ambaye pia ni Mvumbuzi wa Kifaa Maalum cha Kidijitali, cha Kufanyia Upasuaji wa Viungo bila ya kutumia waya (Wireless Arthroscopy Device) Profesa- Dokta Pedro Guillén García (85), amesema ili kuijengea ubora Taaluma ya Afya Duniani, ni vyema kukuza mashirikiano na ujuzi kwa wale waliobobea zaidi katika fani mbali mbali, pamoja na Madaktari wengine wenye ari, hasa wasiokuwa na nyenzo za kutosha, kutoka Mataifa yanayoendelea.

Amesema, kwa upande wa Taasisi yao hiyo, ambayo ni tegemeo Nchini Hispania, hawana-budi kutekeleza Ombi la Serikali ya Zanzibar, kupitia Ziara hiyo ya Mheshimiwa Othman, la kuwaleta Madaktari Bingwa, kuja kuikuza Sekta ya Afya Zanzibar, na ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Akitoa neno la Shukrani kwa Mheshimiwa Othman,  kutokana na Ujio wake Nchini Hispania, pamoja na Ziara yake Hospitalini hapo, Dokta Isabel ambaye ni Mtaalamu na pia Mtoto wa Profesa Pedro Guillén, amesema, wamezunguka kwingi Duniani, kwaajili ya kutoa huduma, bali kwa sasa wanajiandaa kuifikia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, na kwamba wanaipenda na wanaipa heshima ya pekee.

Viongozi mbali mbali wamembatana na Mheshimiwa Othman katika Ziara hiyo wakiongozwa na Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa ambaye pia anasimamia Nchi ya Hispania Balozi Ally Jabir Mwadin, pamoja na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga.

Mheshimiwa Othman, katika Ziara hiyo, ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.




Kitengo cha Habari 

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Novemba 18, 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.