Habari za Punde

Waziri Mhe.Tabia Aagiza Kituo cha Bomba Fm Kufunguliwa

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akizungumza na Viongozi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar na Bomba Fm Redio kuhusiana na kufunguliwa kituo hicho huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita  ameiagiza Tume ya Utangazaji Zanzibar kukifungulia kituo cha Bomba Fm Redio baada ya kufanya marekebisho mapungufu yaliokuwepo.

Ametoa agizo hilo wakati alipokutana na Uongozi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar na Uongozi wa Bomba Fm huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.

Amesema Uongozi wa kituo cha Bomba Fm Redio, umeweza kuyafanyia kazi maelekezo waliopewa na kuiagiza Tume ya Utangazaji kukifungua kituo hicho ili kiweze kuendelea na harakati za Ujenzi wa Taifa.

Hata hivyo amewataka Wamiliki wa Vituo vya Habari kuhakikisha wanafuata Misingi, Kanuni na Sheria za Nchi ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza.

Nae Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Hiji Dadi Shajak ameupongeza Uongozi wa kituo cha Bomba Fm Redio kwa kuyafanyia kazi maagizo waliopewa na Mhe. Waziri jambo ambalo limesababisha kufunguliwa kwa kituo chao.

Hata hivyo amewapongeza Watendaji wa Bomba Fm Redio kwa mashirikiano mazuri walionayo na kuahidi kuendelea kushirikiana ili Viongozi wa kituo hicho waweze kufikia malengo waliojipangia.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Bomba Media Mussa Richard Mwacha na Mkurugenzi Mtendaji wa Bomba Fm Redio Joshua Kisaka wameahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo waliopewa ili kuongeza ufanisi katika Utendaji wa kazi zao za kila siku.

Itakumbukwa kuwa, tarehee 10/12/2024 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita alifanya ziara katika Kituo cha Bomba Fm na kukifungia kurusha matangazo kutokana na kuenda kinyume na masharti ya Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar.

Imetolewa na kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano,

WHVUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.