Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Hanoi, Vietnam kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Aprili 27 hadi 30, 2025.
Akiwasili nchini humo Aprili 27, 2025, kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Noi Bai, Waziri Kombo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Vietnam mwenye Makazi yake Jamhuri ya Watu wa China Mhe.Khamis Omar na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Vietnam.
Waziri Kombo akiwa nchini humo anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wa Ngazi za Juu wa Serikali ya Vietnam kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kuibua maeneo mapya ya ushirikiano, kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi.
Aidha, mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua na kuongeza fursa mpya za uchumi na biashara kwa manufaa ya pande zote mbili, ikiwemo upatikanaji wa soko la bidhaa za mazao ya kilimo na uvuvi yanayozalishwa nchini,uwekezaji, teknolojia na viwanda.
Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo utajumuisha Watendaji na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Sekta binafsi akiwemo Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Gilead Teri, Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi na Biashara ya Kimataifa Balozi John Ulanga na, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bi. Felista Rugambwa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Tanzania na Vietnam zimekukwa na uhisiano mzuri wa kihistoria ambao umechangia kustawi kwa biashara baina ya mataifa hayo mawili. Madhalani, kiwango cha mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Vietnam yaliongezeka kutoka USD milioni 226.6 mwaka 2020 hadi USD milion 314.2 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 38 ndani ya miaka mitano. Vilevile, uagizaji wa bidhaa kutoka nchini Vietnam kuja nchini uliongezeka kutoka USD milioni 20.4 mwaka 2020 hadi USD milioni 60 mwaka 2023.
Kadhali, kwa upande wa uwekezaji Vietnam imewekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo ujenzi, fedha, uzalishaji viwandani, na mawasiliano, ukiwa na jumla ya thamani ya USD bilioni 2.362, ambayo imezalisha ajira kwa takribani Watanzania 226,642.
No comments:
Post a Comment