Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Balozi Maria Manuela Dos Santos Lucas, katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia mawaziri hao pamoja na mambo mengine wamezungumzia namna viongozi wa nchi hizo wanavyoweza kutumia fursa za kidiplomasia kuimarisha ushirikiano wa uwili na kukuza diplomasia ya Uchumi kupitia sekta mbalimbali.
Mhe. Waziri Kombo ameeleza umuhimu wa Tanzania na Msumbiji kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Kilimo cha Mkataba, akikitaja kama fursa ya kimkakati itakayowawezesha wakulima kutoka pande zote kuongeza uzalishaji wa mazao kama korosho na kahawa.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utachangia kukuza usalama wa chakula na kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha Viongozi hao pia wameonesha nia ya kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo madini, biashara itakayokuza Uchumi wa buluu, mafuta na gesi, na kilimo.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Balozi Maria Manuela Dos Santos Lucas, amesisitiza umuhimu wa nchi hizo mbili kuweka mkakati wa kukubaliana maeneo ya ushirikiano kulingana na vipaumbele, ili kuimarisha biashara na uchumi kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wao.
“Tangu tupate uhuru, Msumbiji tumefaidika kwa kujifunza mengi kutoka Tanzania, hasa katika kuimarisha mifumo yetu ya utendaji. Bado kuna fursa kubwa ya kuimarisha mahusiano yetu na Tanzania na kujifunza zaidi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kiongozi imara, anayeendeleza misingi ya utawala bora, umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kukuza mahusiano ya kidiplomasia, biashara, usalama wa kikanda, na maendeleo endelevu”. Alibainisha Mhe. Balozi Dos Santos Lucas
No comments:
Post a Comment