Na Issa Mwadangala.
Wazazi na Walezi Mkoani Songwe wametakiwa kutowachanganya watoto wenye jinsi tofauti katika chumba kimoja ikiwa ni pamoja na kuwalaza chumba kimoja na ndugu, jamaa au marafiki wanaowatembelea ili kuepuka vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na mahusiano ya kimapenzi.
Kauli hiyo ilitolewa Juni 08, 2025 na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban wakati akitoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wazazi/walezi na watoto waliofika kucheza michezo mbalimbali katika Kituo cha kutambua na kukuza vipaji vya watoto kiitwacho Mwakitwange Toto Center kilichopo maeneo ya Isangu Wilaya ya Mbozi ili kujionea mambo wanayoshiriki watoto hao kituoni hapo.
"Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa vitendo vya watoto kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi vinaanzia majumbani ambapo watoto wenye jinsi mbili tofauti wanalala chumba kimoja ikiwa ni pamoja na wageni wanaowatembelea na wakati mwingine hata kitanda kimoja, jambo hilo hupelekea kuanza mahusiano wakiwa wadogo na kuhatarisha mfumo wao wa akili. Pia imebainika kuwa kuchanganya au kuchukua badaboda tofauti tofauti kunapelekea watoto kufanyiwa ukatili pindi waendapo na watokapo shuleni, hivyo niwaombe wazazi mlio hapa kutokufanya hivyo tafuteni bodaboda mmoja mnaemuamini na kumjua vizuri ili endapo mtoto atafanyiwa ukatili iwe rahisi kumbaini mhusika" alisema ACP Akama.
ACP Akama alieleza kuwa watoto wanapoanza vitendo vya mahusiano ya mapenzi wakiwa wadogo hupelekea kutokuwa na mwamko tena wa masomo na badala ya kujingiza kwenye vitendo hivyo na watu wenye umri mkubwa ambapo ndio chanzo cha ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Songwe Mkaguzi wa Polisi Eletisia Mtweve amewataka wanaume kutotelekeza watoto wao kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwa na watoto wa mitaani na ongezeko la watoto kubakwa na kulawitiwa ili wapate mahitaji yao na wakati mwingine hata kusaidia familia.
Naye Koplo Gladness Sizya alisema ni jukumu la kila mzazi/mlezi kuhakikisha anatoa huduma bora kwa mtegemezi wake ili kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto katika jamii ili watoto waendelee kuwa salama na watimize malengo ya masomo na maisha yao ya baadae.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Rita Kamenya amelishukuru kwa dhati Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kushiriki katika tukio hilo na alitumia fursa hiyo kubainisha huduma wanazozitoa kituoni hapo na kuonesha jinsi alivyofurahishwa na elimu iliyotolewa kituoni hapo na ameahidi kuendelea kushirikiana naa Jeshi hilo hasa kwenye mambo ya usalama na ulinzi wa watoto pindi wawepo kituoni hapo.
Pamoja na mambo mengine, ACP Akama aliwasisitiza kutosita kutoa taarifa mbalimbali za uhalifu ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya yao.
No comments:
Post a Comment