Na WMJJWM- New York
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu .
Wakili Mpanju amesema hayo Juni 12, 2025, katika Kikao cha 18 cha Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) ya Umoja wa Mataifa (COSP18) kilichoanza tarehe 10 Juni 2025 jijini New York nchini Marekani.
Wakili Mpanju amesema Tanzania imechukua hatua ya kuunganisha watu wenye ulemavu katika mikakati ya kitaifa ya kupunguza umaskini ikiwemo unafuu wa kodi kwa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, kutoa mikopo nafuu kwa watu wenye ulemavu pamoja na asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu.
"Tanzania chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Mkataba huo na itaendelea kuweka Mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Mkataba huo" amesisitiza Wakili Mpanju
Ameongeza kwamba Tanzania imezindua Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi wa mwaka 2024 – 2027 ambao unatoa mwongozo wa kimkakati kwa sekta zote kuweka mazingira wezeshi ili kila mwenye uhitaji wa teknolojia saidizi aweze kupata kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Wakili Mpanju ameongeza kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinazingatiwa na kuwa msingi wa Usawa wa kijinisia nchini.
Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) ya Umoja wa Mataifa (COSP18) unaangazia juhudi za kimataifa za kuhakikisha usawa na ujumuishaji kwa watu wenye ulemavu.
MWISHO
No comments:
Post a Comment