Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Isaya Arufani Kweka (kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Fred Ilomo, kuhusu elimu ya fedha, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja.
Na. Peter Haule na Joseph Mahumi,WF, Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Isaya Arufani Kweka, ametoa rai kwa Wizara ya Fedha kuendelea kuongeza nguvu ya utoaji elimu ya fedha kwa watanzania wakiwemo watumishi wanaotarajiwa kustaafu ili iwasaidie katika maisha yao.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Jaji Kweka alisema kuwa elimu ya fedha ni muhimu kwa watu wote na ni vema kukawa na mkakati mahususi wa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wote hususani wastaafu ili iwasaidie katika kufanya maamuzi sahihi.
Alisema kuwa wastaafu wengi wanajikuta wanaingia katika mtego wa umaskini kwa kutumia fedha za mafao ya uzeeni bila kuwa na mpango mzuri na kusababisha wazee wengi kujikuta katika mahangaiko makubwa.
Mhe. Jaji kweka amependekeza Wizara ya Fedha kuendelea kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watumishi wa umma na majukwaa mengine kufikisha elimu hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, alisema kuwa tayari mikoa 17 Tanzania Bara imefikiwa na elimu ya fedha mijini na vijijini na Wizara inaendelea kutoa elimu hiyo bila kukoma ili kuhakikisha watanzania wanapata uelewa kuhusu masuala ya fedha.
Alisema kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Mhe. Jaji Kweka ni ya msingi na yamekuwa yakifanyiwa kazi hivyo kumhakikishia kuwa zoezi la utoaji wa elimu ya fedha ni endelevu kwa kuwa jitihada zilizofanyika hadi sasa zimeonesha mafanikio makubwa.
Bw. Mwaipaja alisema kuwa, kulikuwa na wimbi kubwa la watu wanaotapeliwa kupitia mikopo umiza kwa kuwa walikuwa wanakopa bila kujua maana ya mikopo, riba zinazotozwa na wapi wanaweza kuwekeza, lakini kwa sasa elimu kuhusu mambo hayo inatolewa, na tayari shuhuda za mafanikio yake zimeanza kutolewa kwa wanufaika wa elimu katika maeneo yaliyofikiwa.
Aidha, alibainisha kuwa Wizara, kupitia Idara ya Utawala na Rasilimali Watu imekuwa ikiendesha mafunzo kwa wataafu watarajiwa kabla ya miezi sita ya kustaafu kwao pamoja na kutoa elimu ya namna ya kujiandaa kustaafu na kwa waajiriwa wapya.
Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya Sabasaba, limesheheni wataalamu katika nyanja mbalimbali za masuala ya Fedha na uchumi, ambapo wananchi wanapaswa kutumia fursa za maonesho hayo kuongeza elimu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment