Habari za Punde

Singapore yachangamkia fursa za biashara uwekezaji nchini Tanzania

Wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Singapore wameonesha nia ya kuongeza uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara na Tanzania kupita sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo kilimo, nishati jadidifu, viwanda vya kuongezea thamani mazao ya kilimo na uvuvi na uchumi wa kidigitali.

Wameeleza kuwa pamoja na masuala mengine wanalenga kuimarisha biashara kati ya pande hizo mbili, kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi na sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Hayo yamejili kwenye Kongamano la Nane la Biashara kati ya 

Afrika na Singapore (8th Africa Singapore Business Forum – 

ASBF) linalofanyika jijini Singapore kuanzia tarehe 26 Agosti 

2025, ambalo limewakutanisha pamoja viongozi wa ngazi za 

juu serikalini, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za 

kifedha kutoka barani Afrika na Asia.

Kongamano hilo linalohudhuriwa na washiriki zaidi ya 600 kutoka Afrika na Singapore linalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa kibiashara na kiuchumi, kupitia njia mbalimbali ikiwemo ushirikishanaji wa fursa na uzoefu wa biashara na uwekezaji, kuibua na kuchochea miradi ya pamoja ya maendeleo.

Tanzania katika kongamono hilo imejizolea sifa, kuwa ni nchi yenye mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa pana za biashara kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo amani na usalama, sheria na sera rafiki za uwekejazi, faida ya kijiografia inayoiwezesha kuwa kiungo katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, jambo linaloifanya kuwa lango muhimu kwa bidhaa na huduma kuyafikia masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akizungumza na wafanyabiashara, wawekezaji na viongozi wa serikali kwa nyakati tofauti, ameelezea dhamira ya Serikali ya kuendeleza mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia maboresho ya sera na sheria za uwekezaji, huku ikiongozwa na dira ya maendeleo inayozingatia misingi ya ushirikiano wa kimataifa.

Aidha kwa nayakati tofauti viongozi, wafanyabiashara na wawekezaji wa Singapore wameelezea umuhimu wa nafasi ya Tanzania katika kukuza biashara baina ya Afrika na Asia, huku wakionyesha shauku ya mashirika na kampuni zao kutekeleza miradi ya pamoja na Tanzania hususan katika teknolojia ya kilimo, huduma za kidigitali, viwanda na uchumi wa buluu.

Kongamano hilo la Nane la Biashara kati ya Afrika na 

Singapore linafanyika sambamba na mkutano wa Tano wa 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Singapore 

kuanzia tarehe 26 hadi 29 Agosti 2025, huku ujumbe wa 

Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na 

Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit 

Kombo ukijumuisha wafanyabiashara 17 ambao alijumuika 

nao kwenye ufunguzi wa kongamano hilo. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.