Habari za Punde

Vijana Watakiwa Kuitumia Vyema Fursa ya Mafunzo Waliyoyapata ili Kuweza Kujikomboa Kiuchumi Kuachana na Utegemezi.

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya wajasiriamali yaliyotolewa na Shirika la   Youth Challenge International (YCI) Katika ukumbi wa shirika hilo Michenzani Mall.

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab amewataka vijana kuitumia vyema fursa ya mafunzo waliyoyapata ili kuweza  kujikomboa kiuchumi kuachana na utegemezi.

Ameyasema hayo wakati wa kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya wiki nane ya ujasiriamali wa jamii kwa vijana wa kike yanayotolewa na Shirika la   Youth Challenge International (YCI) Katika ukumbi wa shirika hilo Michenzani Mall.

Amesema iko haja vijana kuchangamkia fursa hiyo ili  kufkia ndoto zao jambo ambalo litawasaidia kujisimamia wenyewe katika kuziendeleza biashara zao.

Aidha aliwafahamisha vijana hao kufanyakazi  kwa mashirikiano ya pamoja ili kuengeza uwezo wa kukuza biashara zao.

Katibu Fatma aliwasisitiza vijana hao kutumisha amani  na utulivu wasikubali kutumiwa vibaya hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Shaib Ibrahim Mohamed amelishukuru Shirika la YCI kwa mashirikiano na Serikali juu ya  muongozo  na ushauri wa  kuhakikisha mradi huo unafanyakazi vizuri na kuonyesha mafanikio kwa vitendo.

Kwa Upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Youth Challenge International (YCI) Rose Nzali  amesema vijana hao hupatiwa mafunzo ya wiki nane na kupatiwa fursa ya kuomba ruzuku ambayo inawasaidia kuendeleza biashara zao.

Nao wahitimu hao wamesema wanalishukuru shirika la YCI  kwa msaada wao wa kuwawezesha kujifunza mbinu mbali mbali za kibiashara jambo ambalo limewapa matumaini ya kuweza kujitegemea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.