Na.Habari Afya Zanzibar.
WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikina na Shirika la World Diabetes Foundation WDF katika kupambana na maradhi yasiombukiza hasa Kisukari kwa lengo la kupunguza maradhi hayo.
Akizungumza baada ya kukutana na ugeni huo ulioongozwa na Meneja Mwandamizi kutoka WDF Kanda ya Afrika Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema lengo la kuja kwao ni kuangalia namna Zanzibar ilivyoimarika katika kupambana na maradhi yasiyoambukiza hasa kisukari kupitia misaada wanayoitoa.
Amesema ni miaka mitano sasa shirika hilo limekuwa likifanya kazi na Wizara ya Afya katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na maradhi ya kisukari jambo lililoifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza.
Amesema Zanzibar inaendelea kusumbuliwa na maradhi yasioyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka hasa maradhi ya kisukari ambayo yamekuwa yakaripotiwa kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaougua maradhi hayo.
Amesema kwa sasa Wizara ya Afya imeweka mikakati madhubuti katika kupambana na jambo hilo hasa kwa kushirikiana na mashirika yanayojihusisha na sekta ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa Afya ili kuona jambo hilo linapungua na kuondoka nchini.
Ameongeza kuwa shirika hilo limejiridhisha na miradi inayotekelezwa sambamba na matumizi ya fedha yalivyofanyika katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi ya Kisukari jambo linalotoa fursa nyengine kwa shirika hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar kwa miaka mitano ijayo.
Aidha amesema kufanikiwa kwa jambo hilo ni sehemu kubwa ya utekelezaji wa mkakati wa serikali katika kuona wananchi wanaosumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza hasa kisukari wanapatiwa matibabu stahiki na kwa wakati ili kupunguza idadi ya watu wanaougua maradhi hayo.
Akigusia mpango wa Wizara ya Afya kwa sasa Waziri Mazrui amesema wizara imepanga kuanzisha kambi za matibabu ya Afya katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuweza kupima afya za Wananchi ili kugundua maradhi yanayoendelea kuathiri wananchi kwa sasa.
Hata hivyo amewataka wananchi kufuatilia Afya zao kwa kufanya vipimo katika kambi hizo ili kuchukua hatua stahiki mapema kwa wale watakaogundulika kuwa na maradhi hayo hasa kisukari.
Mbali na hayo amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo na kuyataka mashirika mengine kuangalia fursa za kuisaidia Zanzibar katika sekta ya Afya kwa lengo la kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi kutoka WDF Kanda ya Afrika MADS LOFTAGER MUNDT amesemema ameridhishwa na hatua kubwa inayotekelezwa katika kupambana na maradhi ya Kisukari kupitia misaada yao wanayoitoa hapa nchini.
Amesema katika kufanikisha hatua hiyo wataendelea kuisaidia Zanzibar kuioatia misaada ya kupambana na maradhi yasiombukiza hasa kisukari ili yasiendelee kuathiri jamii ya wazanzibari.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment