Habari za Punde

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI OMBI LA MGOMBEA WA CUF

Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali Ombi la Kikatiba Namba 2 la mwaka 2025 lililofunguliwa na Bwana Hamad Masoud wa Chama cha CUF dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) , aliyekuwa akipinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wa kutomteua kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika hukumu iliyosomwa huko mahkama kuu Tuguu Zanzibar, Mahkama ilieleza kuwa mlalamikaji alipata nafasi ya kusikilizwa kikamilifu kabla ya kuondolewa kwenye orodha ya wagombea, hivyo Tume haikukiuka taratibu za kisheria.

Jaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar Mhe.Ibrahim Mzee Ibrahim  aliyetoa uamuzi huo alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa na Mawakili wa Serikali kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),  umeonesha kuwa Tume, ilifuata masharti yote ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, na kwamba hoja za mlalamikaji hazikuwa na msingi wa kikatiba.

“Mahakama imejiridhisha kuwa mlalamikaji alipewa haki ya kujieleza, na maamuzi ya Tume yalitolewa kwa mujibu wa sheria. Kwa hivyo, ombi hili linatupiliwa mbali,” ilisomeka sehemu ya hukumu hiyo.

Baada ya hukumu hiyo, upande wa Tume ya Uchaguzi ulieleza kuridhishwa na uamuzi wa Mahkama, ukisema kuwa unaonesha uhalali wa taratibu zinazofuatwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Hata hivyo, haijajulikana kama Bwana Hamad Masoud atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Uamuzi huu unakuja wakati maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 29, 2025 yakiendelea, ambapo Tume inaendelea kusisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria na kudumisha amani katika kipindi chote cha uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.