
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zimekutana kwa kikao kazi maalum kinacholenga kuimarisha ushirikiano katika maandalizi na uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, utakaotanguliwa na Uchaguzi wa Kura ya Mapema kwa upande wa Zanzibar tarehe 28 Oktoba 2025.
Akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Jaji Aziza Suwedi, alizipongeza Menejimenti za Tume zote mbili kukutana na kujadili masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao ya kikatiba na kisheria katika kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanikiwa kwa Amani na Haki.
Amesema ushirikiano kati ya Tume hizo mbili ni jambo la msingi lililopewa baraka na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwa kuwa ndio msingi wa kuimarisha demokrasia na kuhakikisha wananchi wote wanapata haki sawa ya kupiga kura.
“Nawapongeza watendaji wote kwa kuja kushiriki katika kikao kazi hiki licha ya kuwa mko katika majukumu mengi ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, ni matumaini yangu mtaweza kujadili kwa kina mambo yote muhimu yatakayosaidia kufanikisha malengo ya Tume zetu na kuendesha Uchaguzi huru na wa haki,” alisema Jaji Aziza.
Aidha, alibainisha kuwa kikao hicho kitajadili namna bora ya matumizi ya vituo vya kupigia kura ili kuwezesha Tume hizo mbili kuendesha Uchaguzi kwa ufanisi zaidi, pamoja na kutatua changamoto ya upatikanaji wa vituo katika maeneo yenye uhitaji mkubwa au uhaba wa vituo vya kupigia kura.
“Naamini jitihada za watendaji Wakuu na Wasaidizi wao mtaweza kutatua changamoto hizi na kufanikisha zoezi la Uchaguzi ” aliongeza.
Kikao hicho pia kimelenga kutoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kiutendaji na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha maandalizi yote ya Uchaguzi Mkuu yanakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.
Jaji Aziza, aliwahimiza washiriki kufanya kikao kwa moyo wa kizalendo, kujadiliana na kushirikiana ili kupata suluhisho la kila changamoto itakayojitokeza.
“Natamani kikao hiki kifanyike kwa moyo wa kizalendo, mshauriane, mjadiliane na hatimaye kuondoa vikwazo vyote katika Uendeshaji wa Uchaguzi. Nina imani kubwa kwamba MTAWEZA NA MTATEKELEZA,” alisisitiza.
Kikao hicho kinahusisha Menejimenti na wataalamu wa Uchaguzi kutoka ZEC na INEC, ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
No comments:
Post a Comment