Na.Mwandishi Wizara ya Afya Zanzibar.
Zaidi ya watu 400 wamepatiwa vipimo na matibabu ya macho katika kambi ya siku moja iliyofanyika katika eneo la mtoni ikijumuisha shehia tano za jimbo hilo.
Zoezi hilo limefanyika kutokana na maombi yaliofanywa na wananchi wa eneo hilo baada ya zoezi lilofanyika siku ya uoni duniani ambapo zaidi ya watu mia mbili walipatiwa miwani na matibabu mengine ikiwemo mtoto wa jicho.
Mratibu wa huduma za Afya macho Zanzibar Dkt.Fatma Juma Omar amesema katika zoezi hilo wameweza kuwapima na kuwapatia miwani Zaidi ya watu mia nne, wakiwemo wanaume themanini(80) na wanawake mia tatu na ishirini(320) na wengine wakipatiwa rufaa katika hospitali ya mnazi mmoja kwa kufanyiwa matibabu zaidi.
Amesema kufuatia uchunguzi walioufanya wameona idadi ya watu wanaokuja katika mazoezi ya upimaji wa afya ya macho wengi wao wanakabiliwa na tatizo la uoni wa karibu na mbali pamoja na mtoto wa jicho hivyo ameiasa jamii kuendelea kutunza afya ya macho kwa kuzingatia kanuni za afya zinazotolewa na wataalamu.
Nae mwakilishi kutoka Shirika la maisha Meds Fadhil Said amesema kupitia shirika hilo wamekuwa wakisaidia jamii kupata vipimo na miwani ya kusomea kutokana na ongeeko la watu wanaosumbuliwa na tatizo la uoni wa karibu na mbali.
Amesema wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Afya Kitengo cha Macho na baadhi ya maduka ya dawa ambapo miwani hutolewa kwa kiwango kidogo cha pesa.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliopatiwa huduma hizo wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na kuwataka wananchi kutumia fursa za matibabu zinazotolewa kwenye jamii.
Wizara ya Afya Zanzibar kupitia kitengo cha macho kimekuwa ikisogeza huduma kwa wananchi za upimaji wa macho na kutoa dawa na miwani bila malipo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment