Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Meli mbili za abiria zinazofanya safari kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara ziitwazo MV. Aziza I na MV. Aziza II zimeteketea kwa moto mjini Zanzibar.
Meli hizo zilianza kuteketea kwa moto saa 10:30 jioni wakati mafundi walipokuwa wakifanya matengenezo huko katika eneo la Mtoni, zinakoendelea kufanyiwa matengenezo.
Meli hizo zenye uwezo wa kubeba abiria kati 870 hadi 1,000 wakati zikiteketea kwa moto zilikuwa ufukweni mwa bahari kwa ajili ya matengenezo yake ya kawaida, ikiwemo kuziba viraka.
Tukio hilo lilisababisha mtafaruku mkubwa baada ya baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la Mtoni kukimbia ovyo baada ya kuona wingu kubwa la moshi likitokea katika eneo hilo, ambapo pia kuna matanki ya mafuta.
Baadhi ya wafanyakazi katika meli hizo walisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea wakati mafundi wakichomelea viraka katika baadhi ya sehemu za meli hiyo.
Moto huo ulianzia kuwaka katika meli ya MV. Aziza I yenye namba za usajili IMO 6806298, baadaye ulirukia katika meli iliyokuwa jirani ya Aziza II, IMO 9372312.
Pamoja na kikosi cha uokozi kufika katika eneo la tukio katika muda mwafaka bado walishindwa kudhibiti moto huo kabla ya kuleta athari kubwa kutokana na uduni wa vifaa. Hata hivyo, Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto Zanzibar, Ali Abdulah Malimusi, alisema kikosi chake kilifanya kazi nzuri, licha ya kukabiliwa na uhaba wa vifaa ambavyo hutumika katika kukabiliana na majanga kama hayo.
Wafanyakazi wa kikosi hicho walilazimika kutumia maji ya bahari katika kukabiliana na moto huo wakiwa na magari mawili ya Zimamoto. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya kuelezwa kwamba yuko katika shughuli ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) huko mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said alitembelea eneo la tukio na kueleza kuwa moto huo umesababisha athari kubwa na utaathiri sekta ya usafiri wa maji Zanzibar.
Hata hivyo, Waziri Machano alikiri ni kweli kikosi cha Zimamoto kinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kisasa vya kuzimia moto, hasa moto mkubwa kama huo, ambao umeteketeza meli mbili kwa wakati mmoja.
Kuteketea kwa meli hizo kutaongeza tatizo la usafiri kati ya Unguja na Pemba, baada ya meli za serikali ya Mapinduzi Zanzibar, MV. Mapinduzi, kukabiliwa na uchakavu na hivyo kushindwa kufanya safari. Meli hizo zilizoungua zinamilikiwa na kampuni ya Mkunazini General Trader ya hapa Zanzibar.
SOURCE: Nipashe
MAFURIKO BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU YAWAKUMBA NGORIKA
-
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
BAADHI ya wakazi wa Kata ya Ngorika wilayani Simanjiro mkoani Manyara,
wamekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kufurika kw...
39 minutes ago
No comments:
Post a Comment