Na Abdi Shamnah
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeliomba Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kuendelea kutoa misaada zaidi ili kuimarisha taasisi za sheria, ziweze kufanyakazi kwa mazingira bora na kufanikisha usimamizi wa sheria na utoaji haki.
Changamoto hio imetolewa jana na Waziri wa Nchi (AR), Katiba na Utawala Bora Ramadhan Abdalla Shaaban na Waziri wa Nchi (AR) Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Othman Nyanga katika mazungumzo maalum na aliyekuwa Mwakilishi Mkaazi wa UNDP nchini Tanzania, Oscar Fernades ambae hivi karibuni ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu msaidizi wa UN anaeshughulikia siasa.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, chini ya Uenyekiti wa Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna ambapo baadhi ya Mawaziri walishiriki.
Aidha mazungumzo hayo yalikuwa na lengo la kumuaga Mwakilishi huyo, ambapo Mawaziri walipata fursa ya kujadili, kuuliza maswali pamoja na kuibua changamoto ili kuona vipi Zanzibar na Wazanzibari wataweza kunufaika moja kwa moja na misaada inayotolewa na mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa, sambamba na miradi inayohitaji kupewa kipaumbele na Shirika hilo, ikizingatiwa kuwa UNDP ni mbia mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar.
Mawaziri hao walisema katika dhana ya Utawala bora, kuna umuhimu kwa UNDP kusaidia gharama za matengenezo ya jengo la Mahakama Kuu pamoja na uwekaji wa samani, kwani fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo hazitoshelezi mahitaji.
Walisema hali ya Vyuo vya mafunzo nchini sio ya kuridhisha, ambapo watuhumiwa pamoja na wafungwa wamekuwa wakilala katika sakafu pamoja na kukabiliwa na matatizo kadhaa ya kiafya kutokana na ukosefu wa madawa.
Aidha waliiomba UNDP kufanya kila juhudi ili mpango wa Serikali wa kupunguza umasikini uweze kupata mafanikio zaidi katika nyanja zote, zikiwemo za kielimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuimarisha sekta ya utalii.
Vile vile Mawaziri hao walizungumzia umuhimu wa Shirika hilo kuendeleza kasi katika utekelezaji wa miradi ya kijamii, ambayo huwagusa moja kwa moja wananchi, na ikiwa ni sehemu muhimu katika mikakati ya kupunguza umasikini.
Aidha waliitaka UNDP kuelekeza nguvu zake za utoaji wa misaada katika uimarishaji wa sekta za habari, utamaduni na michezo, ambazo zilielezwa kuwa ni sehemu muhimu katika dhana ya kupunguza umasikini.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahamoud Thabit Kombo alisema bajeti ya Serikali kwa ajili ya sekta hizo, na hususan michezo ni ndogo sana kufanikisha malengo yaliokususdiwa, hivyo ipo haja kwa UNDP kutoa msukumo ili Zanzibar iweze kufikia lengo la kuwa na wanamichezo wengi katika ngazi ya Kimataifa.
Mawaziri hao walitoa shukurani kwa Mwakilishi huyo kwa mashirikiano makubwa na Serikali na kumtaka kuwa Balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar na kuona kuwa inapata misaada mingi zaidi na ya moja kwa moja.
Mapema Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna aliipongeza UNDP kwa juhudi kubwa inazochukua katika kukiendeleza kijiji cha Milenia, Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, sambamba na uanzishaji wa mradi wa redio jamii unaofadhiliwa na UNESCO, kuwa ni kigezo kikubwa katika kuwaondolea umasikini wananchi wa huko.
Nae Fernandes alipongeza mashirikiano makubwa aliyoyapata kutoa misada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kuainisha kuwa ndio yaliofanikisha ukamilishaji wa miradi mbali mbali ikiwemo ya kijamii na kimaendeleo.
Aliahidi kuwa Balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar na kuhakikisha inajengewa uwezo wa moja kwa moja ili kuweza kutekeleza vyema miradi mbali mbali ya kijamii na kimaendeleo kwa faida ya Taifa na watu wake.
Aidha aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi ilizozichukua kuanzisha Ofisi ya UNDP ndani ya jengo moja na Ofisi za Umoja wa Mataifa, hatua itakayorahisisha kazi za Shirika hilo.
No comments:
Post a Comment