Na Mwinyi Sadallah
Askari 40 wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wameanza kazi ya kuiopoa meli ya MV Fatih kufuatia kuwasili kwa chombo cha kunyanyua mizigo mizito kutoka Tanzania Bara.
Meli hiyo ilizama katika bandari ya Malindi ikiwa na abiria na mizigo. Chombo hicho kiliwasili Zanzibar jana alfajiri na kazi ya uopoaji ilianza muda mfupi baadaye.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja, Bakar Khatib Shaaban, alisema zoezi la uopoaji litaendelea katika eneo hilo kwa vyombo vya ulinzi ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kwa ushirikiano.
Hata hivyo, baada ya wazamiaji hao kumaliza kufunga waya wa chuma na kuanza jaribio la kuiopoa meli hiyo saa 9:00 za jioni, jenereta linalotumika katika chombo hicho cha kunyanyua vyombo vizito, liligoma kuwaka na kuchelewesha zoezi hilo kwa muda.
Wataalam walifanikiwa kuliwasha jenereta hilo na kuanza zoezi, lakini wakati chombo hicho kikianza kunyanyua meli hiyo kutoka chini ya bahari, ghafla waya ulikatika.
Askari hao wa JWTZ wakishirikiana na askari wa vikosi vya SMZ wakiwemo askari wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), walitumia mnyororo kuipoa meli hiyo.
Idadi ya abiria walionusurika katika ajali hiyo imefikia 33 baada ya watu wengine kujitokeza katika ofisi ya maafa.
Hata hivyo, kamati hiyo imesema maiti zilizoopolewa tangu kutokea tukio hilo ni sita tu.
Baadhi ya wazamiaji walisema wanakabiliwa na wakati mgumu wanapozama chini ya bahari kwa vile wanakumbana na giza kutokana na ukosefu wa tochi maalum ya kazi hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment