Nilikuwa nje ya kisiwa cha marashi ya karafuu siku nyingi na niliporudi kwa likizo nikabahatika kupanda daladala.
Daladala ni chombo cha usafiri kinachotumiwa na wakaazi wengi wa kisiwa hiki cha Unguja wasio na uwezo wa kumiliki magari na vyombo vyengine vya kuwarahisishia usafiri wao.
Kilichonipendezesha na kunifurahisha ni kwamba ndani ya daladala tunaweza kujifunza mengi kwa kipindi kifupi cha safari. Mimi nilitoka kutoka kituo cha Michenzani kuelekea Chukwani.
Nikamsikia mmoja wa wasafiri katika safari hii fupi akifanya biashara ndani ya daladala ya kuuza madira. Biashara ilikwenda vizuri mpaka kuweza kupata mteja akiwa ndani ya daladala.
Mwengine amerudi kibaruani na anaonekana kuchoka lakini ni mwenye uso wa furaha. Furaha yake ndiyo iliyonishughulisha kwani vifaa alivoingia ndani ya daladala vilionesha yeye ni fundi bomba.
Ama huyu mmoja ambae aliweza kutushughulisha sote tuliokuwepo ndani ya gari ni mama mmoja ambae mpaka kituo alichokuwa ashuke kinampita na hana habari na aliposhituka na kuomba kushuka huku akimshtua konda, hapo kituo fulani ! Konda alimjibu mbona tumeshakipita hicho kituo!. Alijibu kwa sauti ya huzuni kwamba msinilaumu akili yangu duniani haipo.Jibu lililotoka kwa konda nalo pia lilinifurahisha aliposema: ‘kwani ilikwenda akhera halafu imerudi duniani?’ Mama akajibu ‘ si hivyo yaliyonikuta hamuyajui kwani hivi nnapanda daladala simu yangu ya mkononi imeibiwa ikiwa ndani ya kipochi’
Na huyu mwengine alikuwa akidai chenji yake kutoka kwa konda ya elfu tano huku konda akiwa hana chenji mpaka afike duka na kuomba chenji.
Ni kipindi kifupi cha safari na ukibahatika kupanda daladala yenye mengi basi mengine yatakufurahisha hasa na hizi simu zetu za mkononi. Kwani dada mmoja alionekana akiongea na simu na maongezi yake dhahiri yalionekana katika maongezi ya mapenzi na dhahiri mwanadada alionekana akimdanganya anaezungumza nae kwa kumuahidi mambo ambayo sisi wasikilizaji kutokana na udogo wa kidaladala chenyewe tumeweza kuhisi kana kwamba mwanadada anamghilibu anayeongea nae au kwa ufupi anamtapeli. Na alipomaliza kuongea , bwana mmoja alimuuliza mbona unamdanganya mwenzako? Jibu lililotoka nalo pia lilinifurahisha kwamba, “anapenda kuniudhi na kunikera nami sina budi kumdanganya”
Kwa ufupi sikuwahi kusikia kilichoendelea kwani tayari nilikwisha wasili kituoni kwangu kiembe samaki skuli na hivyo sikuweza kujua hatima ya mwanadada ambae anaonekana kama ana asili ya kibongo.
Niliposhuka nilitafakari yaliyojiri ndani ya safari yangu fupi isiyopungua dakika kumi na tano na kubaini kumbe dala dala si chombo cha kurahisisha usafiri tu bali pia ni chombo muhimu cha kuweza kuufahamu ulimwengu unaotuzunguka.
Ni kweli Daladala ina mengi
No comments:
Post a Comment