CCM itashinda kwa kishindo kikubwa
Asema imefanikiwa kutekeleza ahadi ilizotoa 2005
Ataka Watanzania wamchague, hatowaangusha
Asema CCM ni ya kuaminiwa, kuaminika
Dk. Karume: CCM bado inahitajika kuongoza Tanzania
Amkabidhi Dk.Kikwete, Dk. Bilal ilani ya uchaguzi
Na Mwandishi wetu
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka wananchi wa Tanzania kuipa tena ridhaa CCM kwa kuichagua iongoze Taifa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Dk. Kikwete ambae ni Mwenyekiti wa CCM, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi, uliofanyika viwanja vya Jangwani Mjini Dar es Salaam.
Akishangiriwa na maelfu ya wanachama, wakereketwa, mashabiki na wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, Dk. Kikwete alisema kuwa Chama cha Mapinduzi ni chama chenye kuaminiwa na kuaminika kwa kutekeleza ahadi inazotoa kwa wananchi.
Mwenyekiti huyo wa CCM, alieleza kwamba chama hicho ni chama chenye kuaminiwa na kuaminika kutokana na kutekeleza ahadi inazotoa, kama ilivyofanya kutekeleza Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yameimarishwa katika uongozi wake wa miaka mitano, kuwa ni pamoja na kuimarishwa Muungano wa Tanzania kwa kutatuliwa kero zake na watanzania kuendelea kuishi kwa umoja, mbali ya tafauti zao za rangi, kabila dini na nyenginezo.
Aliitaja amani, utulivu na upendo, kuwa ni masuala yaliyoimarika, ambapo Tanzania imekuwa ikipigiwa mfano duniani na kuheshimiwa kwa kufuata na kuheshimu misingi ya demokrasia, utawala bora, uhuru wa kuabudu, uhuru wa habari na kuwa na mahakama na Mabunge yanayofanya kazi zake kwa uhuru.
Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa baada ya kuimarishwa kwa TAKUKURU, Rais Kikwete alisema Serikali yake itaendeleza vita hivyo kwa kupambana na rushwa ndogo na kubwa kama ambavyo imeanza kufanya.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi, Rais Kikwete amesema Serikali yake imepandisha mishahara ya wafanyakazi, na tayari wameelewana na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na wanafanya kazi kwa pamoja.
Maeneo mengine aliyoyataka kuimarika katika kipindi cha utawala wake kuwa ni pamoja na sekta ya maji, afya, elimu na masuala kadhaa ya kijamii.
Akivizungumzia vyama vingine sita ambavyo vimeweka wagombea katika nafasi ya Urais wa Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa anafurahi kuona kwamba vimenukuu sera za CCM, jambo linaloonesha kuwa hawana kipya cha kuwambia wananchi.
Aliongeza kuvielezea kwamba haviwezi kuikaribia CCM katika kona zote ikiwemo uongozi, sera na hata muundo.
Rais Kikwete aliwataka Watanzania kumchagua tena kuiongoza Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao, na kuahidi kwamba hatowaangusha na atatimiza ahadi zake kama alivyofanya miaka mitano iliyopita.
Dk. Kikwete na Mgombea Mwenza wake, Dk. Mohammed Gharib Bilal, wamekabidhiwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2010-2015, na Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, ili waitumie katika kampeni hizo.
Akihutubia katika mkutano huo, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume amewataka wana CCM na wananchi wote kwa jumla kuendelea kuiunga mkono CCM kwani ndio chama kinachohitajika katika kuliongoza Taifa.
Katika uzinduzi huo ulioanza rasmi kwa upande wa Tanzania Bara, Rais Karume alitoa wito kwa wanaCCM na wananchi kumchangua Rais Kikwete na Mgombea Mwenza, Dk. Mohammed Gharib Bilal pamoja na viongozi wote wa CCM.
Rais Karume amesema kuwa bado CCM inahitajika kuongoza Tanzania, kutokana na ilivyofanikiwa kutekeleza ilani na ahadi zake katika kipindi cha 2000-2010.
Rais Karume alitoa pongezi kwa wanaCCM wa Mkoa wa Dar-es-Salaam pamoja na viongozi wa CCM wa Mkoa huo kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo wa Kampeni za CCM pamoja na kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.
Katika hotuba yake, Rais Karume aliwataka wanaCCM na wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 31 Octoba mwaka huu katika uchaguzi mkuu kwa kuwachagua viongozi wote wa CCM.
“Asiye na mwana aeleke jiwe…..hakuna kusahau wala mchezo, kubwa ni kuhakikisha ushindi kwa CCM”, alisisitiza Rais Karume. Aidha Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na Sera za CCM inaonesha wazi kuwa viongozi wa CCM ni viongozi bora.
Pamoja na hayo, Rais Karume alisema kuwa tayari zana mbili ambazo ni Sera na Ilani za CCM, tayari zipo na zinasubiri utekelezaji kama zilivyo tekelezwa zilizopita.
Katika uzinduzi huo viongozi mbalimbali wa CCM Taifa wa Tanzania Bara na Zanzibar walihudhuria wakiwemo wake wa viongozi hao akiwemo Mama Salma Kkwete, Mama Shadya Karume, Mama Maria Nyerere na wengineo.
Mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais kupitia CCM, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amemshukuru Rais Kikwete kwa kumteua kuwa Mgombea Mwenza wake na kusema ameupokea uteuzi huo kwa furaha na heshima kubwa.
Dk. Bilal, ameeleza kwamba atatumia nguvu, busara na uwezo wake wote kumnadi Rais Kikwete na Ilani ya uchaguzi ya CCM nchi nzima, katika kampeni hizo ili kuhakikisha ushindi unachukuliwa tena na CCM kupitia Rais Kikwete.
Aidha Bilal, alimpongeza Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya CCM na kueleza kuwa atakuwa pamoja nae, kuhakikisha Urais wa Zanzibar unachukuliwa na mgombea wa Chama hicho.
Kabla ya kumkaribisha Dk. Karume, Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Mstaafu Yussuf Makamba, aliieleza hadhara hiyo kwamba tayari chama hicho kimeshashinda katika majimbo kadhaa kiti cha Ubunge, kufuatia Wagombea wake kutopata wapinzani kutoka vyama vyengine.
Ushindi huo unakipa matumaini chama hicho tawala cha kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu utaofanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Makamba aliwataja baadhi ya wagombea hao na Majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Anne Makinda (Njombe Kusini), William Lukuvi (Ismani), Deo Filikunjombe (Ludewa), Celina Kombani (Ulanga Mashariki), Job Ndugai (Kongwa) na Philip Mulugo (Songwe).
Wengine ni Mizengo Pinda (Mpanda Mashariki), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), January Makamba (Bumbuli), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Profesa David Mwakyusa (Rungwe Magharibi) na Gregory Teu (Mpwapwa).
Wakati wagombea hao wakichekelea kuna pingamizi nyingi zimewakabli baadhi ya wagombea, ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika kampeni za uchaguzi mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete natarajiwa kutembelea masafa ya Kilomita 38, 000 nchini kote, ili aweze kuwafikia wananchi wengi zaidi ya alivyofanya katika kampeni za uchaguzi wa Oktoba 2005.
Katika uchaguzi mkuu ujao, wagombea Urais wa CCM ni Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Mwenza wake kwa Tanzania Dk. Ali Mohammed Shein na kwa upande wa Zanzibar ni Dk. Ali Mohammed Shein.
Mbali ya kutumia ndege, Rais Kikwete pia atatumia zaidi gari na helikopta kwa baadhi ya sehemu.
No comments:
Post a Comment