Habari za Punde

VIPAUMBELE 10 VYA SUK 2010 CHINI YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD

MAMBO 10 YATAKAYOKUWA KIPAUMBELE CHA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ITAKAYOONGOZWA NAMI NIKIWA RAIS WA ZANZIBAR

Nimechukua fomu leo hii kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ili niinue juu bendera ya CUF kwa madhumuni ya kuwaomba Wazanzibari ridhaa yao niweze kuiongoza Zanzibar Mpya tuliyoazimia kuijenga. Naamini tutafanikiwa. Lakini nilitaka basi niyataje japo kwa ufupi tu mambo kumi (10) ambayo yatakuwa ndiyo msingi wa maongozi yangu katika kipindi cha miaka mitano ijayo nitakapochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, nikiwa naongoza Serikali ya Umoja wa Kitaiafa, mambo ambayo yatakuwa ndiyo pia msingi wa Ilani ya Uchaguzi ya CUF kwa upande wa Zanzibar. Mambo hayo kumi (10) ni haya yafuatayo:

1 Kuyaendeleza Maridhiano ya Kisiasa tuliyoyaasisi mimi na Rais Amani Karume yakiwa ndiyo njia sahihi ya kujenga umoja wa kweli miongoni mwa Wazanzibari na kuendeleza amani na utulivu uliopo kwa kufuata misingi ya ukweli na mapatano. Katika hili, nitatekeleza matakwa ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyorekebishwa hivi karibuni kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

2 Kuuimarisha Muungano wetu kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuendeleza mazungumzo yenye nia ya kweli ya kuyapatia ufumbuzi wa dhati matatizo yanayoukabili chini ya misingi ya haki, usawa na kuheshimiana baina ya pande mbili zinazounda Muungano huu.

3 Kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mfumo wa soko huria unaotoa fursa ya ushiriki kwa wananchi wote na ambao unaratibiwa vyema na Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wote wanafaidika na fursa hizo na kunyanyua hali zao za maisha katika hali ya neema na tija kwa wote. Sekta za Kilimo, Uvuvi, Utalii, Biashara na Viwanda zitapewa kipaumbele katika ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Zanzibar Mpya.

4 Kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi Serikalini na ubora wa huduma zinazotolewa na utumishi wa umma kwa kusimamia ipasavyo kanuni za kazi, kuwapatia mafunzo ya kazi kadiri inavyowezekana na kuwaongezea mishahara wafanyakazi wetu ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuwa mfano kwa umma.

5 Kwa kufuata mfumo wa uchumi wa soko huria, kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki kwa kutekeleza sera zitakazoweka mazingira mazuri na yanayovutia ya kufanyia biashara na kuleta uwekezaji mkubwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari zetu na viwanja vya ndege vitakavyoweza kutuunganisha na nchi za nje na nchi jirani.

6 Kukiendeleza kilimo na kukirejeshea hadhi yake kama moja ya njia kuu za uchumi inayotegemewa na wananchi wetu walio wengi hasa wa vijijini. Mbali na mazao ya asili yaliyozoeleka, mkazo utawekwa katika kilimo cha viungo, mboga mboga na matunda ili tuendelee kutumia vyema soko linaloweza kupatikana kutokana na jina maarufu la Zanzibar kama visiwa vya viungo.

7 Kuimarisha miundo mbinu na sekta zinazohudumia za uchumi ikiwemo upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme kwa kuongezea nguvu uzalishaji wa umeme wa dharura hapa hapa Zanzibar, kupatikana kwa huduma ya maji safi na salama, na ujenzi wa nyumba za kisasa na za gharama nafuu kwa watu wetu wote wa mijini na mashamba, na kupatikana kwa huduma za uhakika za usafiri wa nchi kavu, baharini na angani. Kipaumbele kitakuwa ni kuanzisha kwa Shirika la Ndege la Taifa la Zanzibar (Zanzibar Airways) ili kuiunganisha nchi yetu na maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara duniani.

8 Kuweka msukumo maalum katika kuinua viwango vya elimu katika skuli zetu za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili Zanzibar iwe ndiyo kituo kikuu cha elimu na mafunzo stadi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mkazo utawekwa katika kusomesha walimu kwa viwango vya kimataifa, kuwapatia maslahi bora ili kuirejeshea hadhi fani na kazi ya ualimu, kuboresha mazingira ya skuli zetu na taasisi za elimu ya juu kwa kuzipatia huduma zote muhimu zinazohitajika kwa ukuzaji wa elimu, kujenga na kuimarisha maabara za kisasa, kutilia mkazo teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA), na kupunguza ukubwa wa madarasa na idadi ya wanafunzi ili walimu waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuipitia upya mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya Zanzibar ya leo kulingana na sera za uchumi tutakazozifuata.

9 Kuinua na kuimarisha huduma za afya katika hospitali, zahanati na vituo vya afya kwa kuweka vifaa vya kisasa vya matibabu, kuvipatia madawa yote muhimu, kusomesha na kuajiri madaktari na wauguzi wapya, kuboresha maslahi ya madaktari na wauguzi, kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhakikisha usafi katika sehemu hizo.

10 Kurejesha maadili mema ya Wazanzibari kwa kuhuisha mila, silka na utamaduni wetu na kuwarejeshea Wazanzibari hadhi na fahari yao iliyotokana na mila, silka na utamaduni huo. Katika kurejesha maadili hayo, Serikali nitakayoiongoza itapambana vikali na uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi visiwani Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa sheria zinatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kudhibiti uingizaji na pia kuanzisha na kuviendeleza vituo vya kuwasaidia waathirika wa madawa hayo ya kulevya ili waache utumiaji huo.


Haya niliyoyaeleza hapa siyo mambo pekee yatakayotekelezwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa nitakayoiongoza. Haya ni mambo nitakayoyapa umuhimu wa kipekee lakini yatajenga msingi wa kuyaendeleza mambo mengine katika sekta na nyanja zote za maisha. Haya na mengine yataelezwa na kufafanuliwa kwa upana zaidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu tutakayoizindua wakati wa kampeni ukifika.

Seif Sharif Hamad
Zanzibar
16 Agosti, 2010

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.