Habari za Punde

ATUHUMIWA KUIBA MIKATE 400 YA BOFLO.

Na Khamis Amani

AFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), imemfikisha mahakamani kijana wa miaka 26, akikabiliwa na tuhuma za wizi wa mikate 400 ya boflo.

Mtuhumiwa huyo Idd Fatawi Idd mkaazi wa Darajabovu wilaya ya Mjini Unguja, amefikishwa mbele ya hakimu Janet Nora Sekihola wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na tuhuma za wizi baada ya kuaminiwa chini ya kifungu cha 267 (1) na 274 (7) (b) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Hati hiyo iliyosomwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka Walid Mohammed Adam alidai kuwa, Febuari 13 mwaka huu, mtuhumiwa huyo aliaminiwa na Sadik Khamis Sadik kwa kupewa mikate 400 yenye thamani ya shilingi 32,000 kwa kukisia.

Alifahamisha kuwa, mikate hiyo alipewa kwa madhumuni ya kwenda kuiuza na baadae kurejesha fedha hizo, lakini matokeo yake hakurejesha fedha wala mikate hiyo.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Kilimahewa wilaya ya Mjini Unguja majira ya saa 2:00 za asubuhi ambalo alilikana.

Walid ambaye ni Mwanasheria wa serikali kuitoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika, na kuahirishwa hadi Oktoba 25 mwaka huu kwa kusikilizwa.

Mtuhumiwa ametakiwa kujidhamini mwenyewe kwa bondi ya shilingi 100,000 pamoja na mdhamini mmoja mwenye vitambulisho aliyetakiwa kuandikisha bondi ya kima kama hicho cha fedha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.