Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ameteua wajumbe wanane wa Baraza la Wawakilishi, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Juma Duni Haji.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ibara ya 66, Rais wa Zanzibar amepewa uwezo wa kuteua watu 10 kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakiwemo wawili kutoka kambi ya upinzani.
Taarifa ya Ikulu Zanzibar iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Abdulhamid Yahya Mzee, imetaja walioteuliwa kuwa ni Juma Duni Haji ambae alikuwa mgombea mwenza wa Dk Ibrahim Lipumba katika kinyan'ganyiro cha kugombea Urais wa Tanzania, na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Fatma Ferej Abdulhabib kutoka CUF ambae alikuwa Mwakilishi wa CUF Mji Mkongwe jimbo ambalo limechukuliwa na mwanasiasa anayekuja kwa kasi Ismail Jussa..
Wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Omar Yussuf Mzee, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano, Balozi Seif Ali Idd na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Zainab Omar Mohammed.
Dk. Shein pia amewateua aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Katiba na Utawala Bora), Ramadhan Abdalla Shaaban, aliyekuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, na Mtaalamu wa masuala ya afya Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya.Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mamboya alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Maradhi ya Kifua Kikuu na Ukoma katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar
Wajumbe hao walioteuliwa na Rais, leo wanatarajiwa kuungana na wenzao 71 kutoka majimboni na viti maalum katika kuchagua Spika wa Baraza hilo pamoja na kuapishwa na Spika huyo.
Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kuanza kwa shughuli ya kumpata Spika kabla ya kuapisha wajumbe wengine wa baraza hilo
No comments:
Post a Comment