JUMATANO, NOVEMBA 17, 2010
BISMILLAH RAHMANI RAHIM
Natanguliza shukurani kwa Mwenyezi Mungu, alietujaalia uhai na akatupa muongozo wa kuwa waumini kwake. Sifa na shukrani zote ni zake na Yeye ndie Muweza wa kila kitu. Swala na salamu zimshukie Mtume wake, Sayyidna Muhammad (SAW) alieletwa kuwa Rehma kwa walimwengu wote, Rehma ziwashukie wazee wetu, ndugu, marafiki na jamaa zetu waliotutangulia mbele ya haki - Amin. Mwenyezi Mungu atubariki katika siku hii na nyengine zote.
Sheikh Khamis Haji Khamis,Naibu Kadhi Mkuu;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Kwanza wa Rais;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Hamid Mahmoud Hamid, Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho,Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Waheshimiwa Mabalozi Wadogo wa Nchi za Nje,
Waheshimiwa Masheikh;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
ASSALAM ALEYKUM,
IDD MUBARAK
Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu Subhaanahu Wata’ala, natoa shukurani kwake kwa kutujaaliya afya na uzima tukaweza kufika hapa leo kusherehekea sikukuu kubwa aliyoainisha yeye mwenyewe kwa Waislamu. Pia, namshukuru kwa kutujaalia amani na salama nchini mwetu.
Mola wetu, kwa hekima yake, ametuwekea sisi Waislamu sikukuu mbili katika mwaka, nazo ni Idd el Fitr - sikukuu ndogo na Idd el Hajj - sikukuu kubwa. Zote zinathamani yake kwake Mola wetu na tumeamriwa tuzisherehekee kwa utaratibu wake, na kila moja ina maana na mafunzo kwetu binadamu.
Kuhusu sikukuu kubwa, Mola wetu alimuagiza Mtume wake Sayyidina Muhammad,(S.A.W) kwa kumwambia:
“Hakika tumekupa kheri nyingi: Basi sali kwa ajili ya Mola wako, sala ya Idd, na uchinje mnyama – kwa ajili ya Mola wako”.
Hilo ni agizo la kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kheri alizompa binadamu.
Ndugu Wananchi,
Leo tumekusanyika hapa kusherehekea kwa pamoja Idd el Hajj. Mkusanyiko wetu huu wa kupendeza, unathibitisha kwetu uhakika wa kheri ambapo Mola wetu ametupa na moja katika kheri kubwa ambazo waislamu tumejaaliwa nazo ni ule umoja na udugu wa umma wetu kama unavyojidhirisha huko Makka, Arafa na Mina katika ibada ya Hijja. Mtume wetu Muhammad (S.A.W) ametuambia:
“Hakika waislamu wote ni ndugu”
Vile vile, alitilia mkazo udugu huo katika hotuba yake ya Arafa, alipovunja imani za watu kubaguana.
Umoja unaoonekana wazi wazi katika siku za Hijja ni mafunzo kwetu wanadamu kutoka kwa Muumba wetu kutaka tuishi na tufanye shughuli zetu za kheri kwa pamoja. Ni ujumbe mzito wa Rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu wetu kupitia kwa Mtume wake Sayyidna Muhammad (S.A.W).
Katika umoja huo inapatikana sifa kubwa kwa wenzetu wanaohiji kuwepo amani, ustahamilivu na upendo baina yao. Mambo hayo yanawawezesha kukamilisha ibada zao za Hijja kwa mafanikio makubwa na kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Hili ni funzo kubwa kwetu kwamba penye umoja panakuwepo amani na pia mapenzi kati ya watu na hivyo hivyo bila ya amani umoja hauwezekani.
Ndugu Wananchi,
Ni jambo la faraja kwamba nchini mwetu tokea kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa Novemba 5, 2009, wananchi wamekuwa na moyo mmoja wa kupenda umoja na kushirikiana. Hayo yalidhihirishwa katika Kura ya Maoni ya Wazanzibari ambao kwa sauti ya wengi walitaka umoja. Wachambuzi wa mambo wanasema sababu moja kubwa ya hatua hiyo ni kutaka amani ndani ya nchi, kwani matunda ya umoja, kokote duniani ni kuwepo kwa amani. Tumeshuhudia haya na, pia, kwa kuwa na umoja tumeweza kufanikisha mambo mengi. Kwa kuwa sote tunakubali umuhimu wa umoja na mshikamano, lazima tukubali umuhimu wa amani ambayo ndiyo inayotunza na kudumisha umoja huo. Napenda kusisitiza haya na kuwataka viongozi na kila aitakiae mema nchi yetu ahubiri kwa vitendo na aendeleze umoja na amani.
Ndugu Wananchi,
Kwa mnasaba wa sikukuu hii ya Idd el Hajj ni vyema vile vile tutafakari na kujifunza mambo mengine zaidi ya umoja ambayo yanaambatana na msingi wa sikukuu hii. Yapo mambo mawili katika mnasaba huu, nayo ni utiifu na kujitolea nafsi, mambo ambayo yamo katika kila hatua ya ibada ya Hijja.
Sherehe ya Idd hii, kama tunavyojua, inatokana na kisa cha Nabii Ibrahim, (A.S.) cha kuazimia kumchinja mwanawe, Sayyidna Ismail (A.S.) na kuridhia kwa Sayyidna Ismail. Vitendo vyao wote wawili ni uthibitisho mkubwa wa utiifu. Nabii Ibrahim alionesha utiifu kwa Mola wake na Sayyidna Ismail akaonesha utiifu kwa Mola wake na baba yake.
Hapa tunaona kwamba utiifu ni funzo kwetu binadamu kutoka kwa Mola wetu. Kama ilivyokuwa dahari zilizopita katika maisha ya mwanadamu na hata katika maisha yetu ya leo, utiifu umekuwa ni chanzo cha kuleta mafanikio na kujenga jamii zenye desturi nzuri na mambo mema mengine. Utiifu ni kwa kila daraja ya watu, watoto, watu wazima, wanafunzi, walimu, madaktari, askari, wafanyakazi na kadhalika katika jamii.
Tukianza kwa watoto, utiifu wao kwa wazazi ni jambo la msingi. Watoto wafunzwe na kuendelezwa kuwa watiifu kwa Mwenyezi Mungu, mila, desturi na silka za jamii yao. Kufanya hivyo kutawafunza watoto kuwa na tabia nzuri na kujikinga na maovu, kama vile matumizi ya madawa ya kulevya na hatimaye kuingia katika janga kubwa la ukimwi na maradhi mengine. Vile vile, itawafanya kuwa raia wema na washiriki katika vikundi vyenye kuwapa manufaa na mafunzo bora ya kijamii. Wazazi wafuatilie nyenendo za watoto wao wakiwa skuli na wakiwa nje ya skuli. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tokea kuasisiwa kwake kutokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964, imekuwa na sera na mipango kadhaa ya kuwalinda watoto pamoja na kuwapa haki zao na kuwafunza umuhimu wa utiifu. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, awamu ya saba, imepanga kuendeleza msingi huu kwa watoto ili kuimarisha maendeleo yao na haya yameelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 na tutayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ndugu Wananchi,
Nayazungumzia haya katika sherehe za Idd kwa sababu ni mambo ambayo yanafaa tuyachukulie kwa umuhimu wake katika sera na vitendo vyetu vyote wakati wote. Utiifu, kwa mfano, ndio uliotufanya sote hapa tuitukuze na tuisherehekee siku hii pamoja na swala ya Idd na kuchinja.
Ni jambo lililo wazi kwamba pamoja na kuwafunza utiifu watoto wetu, sisi wenyewe lazima tuweke mbele utekelezaji wake na kuuheshimu utiifu, kuanzia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, viongozi wetu na kwa wote waliopewa dhamana juu yetu, makazini mwetu hadi kwenye jamii zetu. Mwenyezi Mungu ametuambia katika kitabu chake kitukufu Kurani kuwa: (katika Suratu – Nnisaa Aya ya 59)
“Enyi mlioamini, mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini
Mtume na wenye mamlaka juu yenu ….”
Utiifu kazini ni msingi wa kujenga uadilifu na mwendo wa kazi unaoleta ufanisi na maendeleo. Wakati huo huo, nchi hustawi na kuwa tulivu kutokana na wananchi wake kuwa watiifu wa sheria za nchi yao na kanuni zinazotawala jamii. Maendeleo mazuri yanapatikana pale ambapo wananchi wana umoja na watiifu kwa nchi yao, na wanaheshimu amani na utulivu. Natumai haya yatakuwa ni mambo ambayo sote tutayazingatia katika maisha na shughuli zetu za kuendeleza nchi yetu na kuendelea kuijenga Zanzibar.
Katika hotuba yangu ya kulizindua Baraza la Nane la Wawakilishi, nilizungumzia kwa urefu malengo tuliyopanga kuyafanya ya kuiendeleza nchi yetu. Katika kuyafikia malengo hayo tunahitaji tuwe na imani thabiti ya umoja na utiifu. Tunalazimika kujenga na kuthamini maadili ya Kizanzibari ambayo yatatuwezesha kufuata njia sahihi ya kufikia kwenye malengo yetu kwa kujali na kuheshimu mambo niliyoyasema hapo awali. Pamoja na hayo, napenda kusisitiza pia umuhimu wa kuwa na maadili mazuri katika jamii.
Ndugu Wananchi,
Katika kuendelea kuijenga Zanzibar ili ipate maendeleo zaidi na katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo, tunapaswa tuizingatie misingi ya uadilifu na kuitekeleza. Katika uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi hapo tarehe 9 Novemba, 2010, niligusia dhamira ya serikali yangu katika kupiga vita maovu katika jamii, kwa mfano, kupambana na rushwa, ambayo ni kinyume cha maadili yetu. Natilia mkazo dhamira hiyo kama ninavyoukazania umoja na amani nchini, kwa kila mmoja awe tayari kufanyakazi kwa upeo mkubwa na bidii zaidi kwa kuzingatia kanuni za utumishi na taratibu nyengine ziliopo.
Ndugu Wananchi,
Leo si siku ya kuzungumza kwa kutoa hotuba ndefu, ila nasema tusherehekee Idd yetu kwa kuzingatia sana mafunzo ambayo yamo katika ibada hii ya Hijja na kuyatumia katika ujenzi na maendeleo ya nchi yetu. Namalizia kwa kueleza furaha yangu kwa wale wenzetu, jamaa au marafiki, waliofanikiwa kwenda kuhiji mwaka huu. Napenda kutoa pongezi kwa taasisi zilizotayarisha safari za Hijja lakini napenda kutoa wito kwa watayarishaji kuwa na ushirikiano na umoja mkubwa zaidi katika jambo hili. Pengine jambo hilo litasaidia katika kupunguza gharama za usafiri kwani ni tatizo kubwa kwa wanaotaka kwenda kuhiji na kuwaondolea shida nyenginezo. Mifano ya kuiga ipo kwa nchi nyingi; kwa mfano Indonesia, Misri, Sudan na Malaysia. Tusichukulie jambo hili jema na la kheri kuwa ni ushindani. Quran inatuhimiza kushirikiana katika kufanya mema na huu ndio umoja tunaohimizana.
Wakati huo huo, ninafuraha kubwa kwa kusikia kuwa mahujaji wetu wapo salama na wanaendelea vyema na ibada zao. Tuungane kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awawezeshe kumaliza ibada zao zote kwa kheri na salama, na warejee nchini salama usalimini. Tukiwasiliana nao, tuwatake watuombee sisi na nchi yetu kheri na baraka.
Ndugu Wananchi,
Nafahamu watu wengi leo watachinja wanyama kwa ajili ya kutekeleza aliyoamrishiwa Bwana Mtume kuchinja. Hatua hiyo itatuwezesha kusherehekea Idd vyema na katika hali ya umoja. Sababu moja ni kwamba mnyama tunaemchinja, tunapaswa tutoe thuluthi moja kama sadaka kwa masikini na wasiojiweza ili nao waweze kufurahikia Idd.
Tunakumbushwa uadilifu kwa kufikiria ndugu na jamaa zetu kwa kuwapa fungu la pili la nyama hiyo. Bila ya kujisahau kujifurahisha wenyewe, tumeagizwa fungu la tatu kufurahikia Idd. Haya ni maagizo ya uadilifu na ambayo kwa kuyafuata yanatilia nguvu umoja, upendo, na kusaidiana katika jamii.
Ndugu Wananchi,
Tushirikiane katika kusherehekea Idd kwa mazingatio ya kutilia nguvu umoja na mshikamano wetu, kuendeleza na kudumisha amani.
Sherehe zetu ziwe za amani na kuzingatia maadili na utamaduni wetu. Si vyema kwa mtu au watu katika kusherehekea akawaudhi au akawadhulumu wengine. Tudumishe ustaarabu wetu wa kawaida wa kufurahi kwa pamoja na bila ya fujo.
Wafanyabiashara nao wasitumie fursa hii ya furaha kupandisha bei za vyakula na vinywaji baridi pamoja na vitu vya kuchezea na huduma za watoto kwa kuviuza kwa bei ya juu ambapo itawafanya baadhi ya watoto wengine wajione wanyonge kwa kutovimudu vitu hivyo kuvinunua.
Aidha, napenda tushirikiane katika kufanya mambo mema ya kuwapa furaha na faraja masikini miongoni mwetu, wagonjwa na watu wasiojiweza. Tuwe waangalifu njiani na watumiaji wa vyombo vya moto na wengine wawe na hadhari zaidi barabarani.
Mwisho, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwenu nyote kwa kuitikia mwaliko wa kuhudhuria Baraza hili la Idd el Hajj na pia nawashukuru wote ambao wanafuatilia sherehe hizi katika vyombo vya habari. Nawashukuru waumini wa dini nyengine ambao wamekuja kusherehekea pamoja na sisi. Huu ndio moyo na mfano mzuri wa umoja wetu Wazanzibari.
Kwa niaba ya familia yangu na mimi mwenyewe, natoa salamu za Idd kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania Bara, viongozi mbali mbali nchini mwetu na kwa kupitia Mabalozi wa nje waliopo hapa tunatuma salamu za Idd kwa viongozi na ndugu zetu wa Kiislamu katika nchi zao. Aidha, tunawatumia salamu Wazanzibari na Watanzania wote walioko nje ya nchi kwa wakati huu. Tunawatakia wote Idd ya kheri furaha na amani.
Idd Mubarak
Kullu Aam Waantum Bikheir na Ahsanteni sana.
No comments:
Post a Comment