Habari za Punde

DK SHEIN AKUTANA NA WATENDAJI WAKUU WIZARA YA ELIMU, ARDHI

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Ali Mohamed Shein ameeleza haja ya kuwajengea mazingira mazuri waalimu wa maandalizi, msingi na Sekondari ili kuhakikisha elimu wanayoitoa kwa wanafunzi inaleta tija na kukidhi haja kwa wakati uliopo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ikiwa ni hatua ya kuzungumza na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kuwa sekta ya elimu itapata mafanikio makubwa na kuahidi kufanyiwa kazi changamoto mbali mbali zilizopo.
Katika mazungumzo hayo, pia Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwa na programu nzuri kwa ajili ya maandalizi kwa watoto kwa kuweza kutoa mafunzo kwa walimu wa maandalizi na kueleza kuvutiwa na mpango wa Wizara hiyo wa kuwasomesha walimu wa maandalizi kwa njiaya redio.

Alieleza kuwa ni vizuri kwenda sambamba na wakati uliopo kwa kuwafundisha vizuri waalimu wa skuli za maandalizi, msingi na sekondari.

Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuunda Taasisi ya Elimu ambayo miongoni mwa malengo yake ni kuondoa changamoto mbali mbali zilizopo katika sekta ya elimu.

Pamoja na hayo alieleza mikakati ya kuongoza vifaa mbali mbali katika skuli za Zanzibar vikiwemo vikalio na vifaa vya maabara.

Pia, Dk. Shein alieleza umuhimu wa Wizara kuhakikisha skuli na majengo ya vyuo yanapata hati miliki na kuweka mipaka ili kuyakinga majengo na maeneo hayo kutovamiwa kiholela.

Dk. Shein alisifu hatua na mipango ya Wizara ya Elimu ya kumaliza majengo ya skuli yanayojengwa na wananchi na kuahidi serikali kuendelea kuunga mkono juhudi hizo za wananchi.

Alieleza haja ya Wizara ya Afya, Elimu pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kukaa pamoja ili kubuni uanzishwaji wa kada ya ‘Udaktari’(Faculty of Medicine) katika Chuo Kikuu cha SUZA.

Sambamba na hayo alieleza umuhimu wa mawiyano na mahitaji ya wanavyuo wa Vyuo Vikuu, ili kuepuka matatizo katika soko la ajira.

Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa kuwepo mwenendo na uratibu wa kufanya tafiti mbali mbali zitakazosaidia maendeleo ya nchi na kueleza kuwa Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais ndio itakayokuwa msimamizi wa shughuli hizo.

Katika Kikao hicho, Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Iddi alihudhuria na kueleza haja kwa viongozi wa Majimbo hasa Wabunge kutoa michango yao kwenye kasma maalum wanayopewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kwa kuweza kusaidia uimarishaji wa sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Nao viongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu walieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo na changamoto zinazowakabili pamoja na mikakati waliyoiweka katika kupambana na changamoto hizo.

Waziri wa Elimu Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban alieleza hatua mbali mbali zilizofikiwa na sekta hiyo katika kuhakikisha suala zima la elimu linapata mafanikio makubwa. Aidha, Waziri Shaaban alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara hiyo katika kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafanikiwa.

Dk. Shein pia, alifanya mazungumzo na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na kueleza matumaini ya wananchi waliyonayo juu ya Serikali yao katika kuhakikisha wanapata huduma muhimu.

Katika kikao hicho Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwapatia wananchi huduma muhimu ikiwemo maji, umeme pamoja na kuwajengea mazingira bora ya makaazi ya kuishi.

Alieleza azma ya Serikali katika kuhakikisha changamoto mbali mbali zilizopo katika huduma hizo kufanyiwa kazi ili kuwawezesha wananchi kuimshi maisha bora zaidi.

Nao wafanyakazi wa Wizara hiyo walieleza mafanikio, changamoto na mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha huduma hizo muhimu kwa wananchi zinakwenda sawia.

Walieleza kuwa licha ya changamoto zilizopo lakini pia, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuimarisha sekta hizo muhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.