Leo mchana, Zanzibar Heroes itaingia tena dimbani kupambana na The Cranes ya Uganda katika mchezo wa robo fainali kugombea kombe la Chalenji.
Zanzibar Heroes walotolewa na Uganda 2-1 katika mashindano haya mwaka jana katika hatua ya Nusu fainali. Ila walipopambana katika hatua za makundi ziliweza kutoka suluhu bila ya kufungana. Timu hizi zimeshawahi kukutana mara 34 katika mashindano na bado Wazanzibari wana kumbukumbu nzuri ya mwaka 1995 ambapo tuliweza kuwafunga Waganda nyumbani kwao 1-0 katika mchezo wa fainali na kuchukua Kombe.
Kocha wa Zanzibar, Stewart Hall alisema "Uganda ni mabingwa watetezi, tunawaheshimu, lakini hatuwahofii naamini kikosi changu ni bora katika mashindano haya, makosa machache yaliyokuwa yanafanywa na wachezaji wangu siyatazamii leo."
"Mechi zilizopita tulitengeneza nafasi zaidi ya mara tano, lakini washambuliaji wangu walishindwa kufunga magoli, siwalaumu kwa hilo kwa vile wengi hawajawai kucheza mechi za kimataifa na pia wingi wa mashabiki unawachanganya."
Kikosi cha Timu ya Zanzibar Heroes kinajengwa na mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na mashindano makubwa kama Abdi Kassim, Nadir Haroub, Sabri Ramadhan na Abdul halim Humoud pia ina wachezaji ambao bado wanachipukia katika medani ya soka la kimataifa kama Ally Ahmed Shiboli, Khamis Mcha na wengineo ambao wanashiriki mara ya kwanza katika mashindano makubwa.
Tuiombee dua timu yetu iweze kulipiza kisasi leo na pia kuonesha kwamba baada ya miaka kumi na tano tokea kulibeba kombe la chalenji, tunaweza kufanya lile ambalo tulilifanya 1995 na kulibakisha kombe
No comments:
Post a Comment