Na Ally Saleh,
Naandika makala hii kwa hadhari ya kwamba pengine wakati makala hii inatokana kile ambacho ninakusudia kukiandikia kitakuwa kimeshafikia hatua ya maamuzi, yaani Rais Dk Ali Muhammed Shein ameshachukua hatua inayomstahikia kikatiba.
Na kwa hakika mamlaka aliyonayo kikatiba ni yake peke yake, na sisi sote tunaopiga kelele na hata wale wanaomshauri wanafanya hivyo kwa kuwa ni wajibu wao, lakini hatimae ni yeye ndio mwenye kuamua.
Ila maamuzi yake kama Rais ingawa ni ya kisheria na kikatiba, kwa maana ya uhalali na kuwa na mashiko ya nguzo kuu ya utawala, lakini haina maana kwamba maamuzi hayo hayawezi kukosolewa au kulalamikiwa.
Yatakoselewa na kulalamikiwa kwa sababu ya kutegemea na tukio lenyewe. Kutegemea huko kutakuja iwapo Rais amefanya maamuzi yoyote yale sio tu kwa mujibu wa katiba na sheria lakini pia iwapo maamuzi hayo yamefanywa akiwa na taarifa za kutosha.
Mara nyingi ni ukosefu huu wa taarifa ndio unaoweza kumpelekea Rais au mtu yoyote mwenye kufanya maamuzi kufanya maamuzi mabaya au tuseme mabovu na kama nilivyosema hata yawe ni kwa mujibu wa sheria au katiba basi yanaweza kulalamikiwa.
Maamuzi ya Rais kwa mfano kuchagua mtu kushika nafasi fulani mara nyingi huwa ni ya mchakato. Ni mara chache Rais hufanya maamuzi yanayofanana na haya moja kwa moja na kuna sababu moja kubwa katika jambo hili.
Rais hawezi kuwajua watu wote katika nchi yake na kwa hivyo hawezi pia kujua uwezo wa ki-elimu na kiutendaji wa watu wake wote aqu hata watu ambao ana uwezo wa kuwachagua ambao si moja kwa moja raia wa nchi yake kwa baadhi ya ajira kwa mfano katika Idara ya Mahakama.
Bila ya shaka hapa lazima tutofautishe au tuelewe juu ya baadhi ya nguvu za uteuzi za Rais ambazo hufungwa katika masharti na ambapo nyengine haina masharti ingawa hata hivyo sharti la kupata ushauri mwanana na usiolalia upande wowote lina umuhimu unaopita uzito wa mizani.
Sasa iwapo Rais ameshauriwa vibaya au utaratibu wa uteuzi umekuwa na mashaka kwa kuwa mizani haikutumika sawa sawa inakuwa ni mtihani mkubwa kwa kiongozi kama huyo kufanya maamuzi.
Bila ya shaka waliojua kuwa utaratibu umekiukwa wakinyamaza kimya watakuwa wanafanya kosa na kosa kubwa zaidi litkuwa kwao kuja kusema wakati maamuzi yameshafikia hatua ya mwisho kwa mfano mapendekezo ya kuteua majaji wa mahakama kuu yakifikia hatua ya majaji hao kuapishwa.
Walio katika rubaa za kisheria wanajua fika athari ya kumuapisha jaji. Kinyume na kada nyengine ambapo kama utaratibu haukufuatwa au kama kumetokea makosa, Rais aweza kufuta uamuzi wake, lakini katika kada ya ujaji hilo ni gumu mno.
Kisheria na kikatiba si rahisi kumvua jaji madaraka. Huwa ni kama kazi yake ya maisha na katiba inaelekeza utaratibu wa kuunda kamati kumchunguza, lakini katika hili kamati ingekuwa ya maana gani wakati hapana kosa lilofanywa na majaji kwa maana kama ni kosa basi si lao kwa sababu wao sio waliojichagua.
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibut tokea kuzuka kwa sakata la mapendekezo ya majaji ambao Rais Dk Shein amependekezewa kuwachagua na Kamati ya Uajiri ya Mahakama na kuvutiwa na hatua ya kishujaaa iliyochukuliwa na Chama cha Mawakili cha Zanzibar (ZLS) kumzindua Rais juu ya kile walichokiona ni uwezo mdogo wa baadhi ya wapendekezwa hao.
Bila ya shaka pia ZLS wamemzindua juu ya utaratibu mbaya au kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupendekeza majaji hao ambapo waliolalamikiwa ni Fatma Hamid Mahmoud na Mkusa Issac Sepetu huku wengine wakielezwa kutokuwa na matatizo ya kiuwezo na kiutendaji.
Kwa hakika hoja ya ZLS ni nzuri sana. Kwamba ni wao wanasheria wataofanya kazi nao, yaani hao majaji, na kwa kuwa nchi hii ni yao na wao ni wadau, basi wakaona ni kheri wamzindue Rais kabla mambo hayajakorogeka.
Pengine hili halikupokewa vyema na wahusika, lakini hali hii inaweza kuelekeweka kwa sababu wao kama binaadamu au watu binafsi, wanaweza kuona kuwa wamekoseshwa ulaji au hata fursa ya kutumikia umma, ila kwa maana ya picha ya kitaifa basi wangezingatia hatua hiyo ina umuhimu kuisaidia jamii na sio kuwakomoa wao.
Wengi tunashukuru kuwa wamejitokeza au kimejitokeza kikundi ambacho kimeweza kuja mbele na kukosoa jambo hilo, na kitu kama hicho kikiwa ni kipya katika utamaduni wa kisiasa wa Zanzibar. Ni wachache kati yetu ambao sio tumekuwa na mwamko bali hata moyo wa kufanya hivyo.
Wengi wetu tunaamini juu ya usafi na nia njema za taasisi zetu hata katika nyakati kama hizi za kupendekeza majina kufanyiwa uamuzi na Rais, lakini kwa hatua ya ZLS tumeona na kunaweza kumzinuda Rais kukaa makini katika mambo kama hayo. Kumbe si majina yote anayopelekewa ndio yenye uwezo au uzoefu wa nafasi zinazopendekezwa afanyie uteuzi.
Hadi sasa binafasi sijasikia lolote katika vyombo vya habari kuhusu kauli za majaji watarajiwa yanaolalamikiwa. Pengine uamuzi wa kukaa kimya ni wa busara kwa sababu unaepusha majibizano ya hadharani na ambayo si mazuri kwa wafanyakazi wa taasisi kubwa kama hiyo ya mahakama.
Lakini naamini kuwa ufunguo wa kumaliza tatizo hilo na kumsaidia Rais lipo kwa majaji watarajiwa wanaolalamikiwa na ZLS bila ya kujali au kutafuta visingizio iwapo waraka wa chama hicho umesainiwa na nani na nani au kuanza kutafuta vipenyo vyengine kama iwapo kuanza kuleta hisia kuwa hawapendwi au wanaonewa chuki.
Majaji watarajiwa wakue kimawazo, wakue kisheria na wakue kizalendo. Nafasi ambazo wangepewa zisingekuwa zao binafsi kama Fatma na Mkusa bali zilikuwa ni za umma na kutumikia wananchi. Washukuru maoni juu yao yamekuja hivi mapema, kuliko wangeanza kupigwa vita na kugomewa wakati wakiwa vitini. Wasifikiri maslahi yaliokuwa yaje mbele yao, ila wafikirie ingekuwaje mawakili waakanza kuwapima uwezo wao kihasira wakati wakishakuwa vitini. Kujenga bifu isiyo na lazima.
Kwa fikra zangu ni kuwa Fatma na Mkusa wangejitoa. Wana nafasi kubwa ya kumuandikia Rais Dk Shein na kumwambia kuwa wangethamini uamuzi wake wa kuwateua kwenye nafasi hiyo ya heshima, lakini wanaamua kuyaondoa majina yao.
Hii haitakuwa na maana ya kushindwa maana hapa hapakuwa na ushindani. Kwa sababu Fatma na Mkusa wajue kuwa nchi ni kubwa kuliko wao na wakubali ukweli kwua ingekuwa vigumu kwao kufanya kazi katika mazingira yaliokuwa yamejitokeza.
Tushukuru mpaka naandika makala hii, Rais Dk Shein alikuwa hajamuapisha yoyote katika ya majaji waliokuwa wamependekezwa kwake na huku nikiamini kuwa Rais amekuwa akiendelea kufanya mashauriano katika suala hili na huku nikiamini kuwa Dk Shein hatakuwa “kichwa ngumu” katika hili maana athari yake katika rubaa ya kisheria na utoaji wa haki itakuwa kubwa mno.
Ndipo nikasema kila kitu kinaweza kikawa rahisi iwapo Fatma na Mkusa watakubali ukweli. Na ukweli katika hili ni kwamba nafasi hizo za ujaji kwa sasa kwa wao hazingewafalia na barua ya mstari mmoja kumpelekea Rais itajenga heshima kubwa kwao kupita kiasi.
Nitashukuru watu wanaowashauri (mentors) wawatie busara hii katika akili zao. Wote bado ni vijana na wana muda wa kukua katika kazi hiyo na kuiva sawa sawa. Wakosapo kuteuliwa ujaji leo sio mwisho wa safari kama vile wakosapo nafasi hiyo kabisa sio mwisho wa maisha.
Fatma na Mkusa kuweni watu wazima na mukubali kuiepusha fani ya sheria na nchi kuingia katika mgogoro ambao mnaweza kuuepusha nyinyi wenyewe kama wananchi na wazalendo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment