Habari za Punde

WAZIRI APIGA MARUFUKU MELI ZENYE INJINI MOJA

Na Mwantanga Ame

WAZIRI, wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Massoud, amezipiga marufuku meli zote zinazofanya safari zake katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kutumia injini moja.

Tamko la Waziri huyo linakuja baada kujitokeza kwa lawama za wananchi ambao walisafiri na Meli ya M.V Serengeti kutoka kisiwani Pemba kuja Unguja kukaa baharini kwa masaa kadhaa.

Wananchi hao walisafiri na meli hiyo kutoka kisiwani Pemba waliondoka saa 3.00 za asubuhi lakini walifika Unguja 2.00 za usiku baada Meli hiyo kuharibika njiani moja na kulazimika kutumia injini moja.

Hali hiyo iliwafanya baadhi ya abiria kulalamikia meli hizo na kuitaka Serikali kuingilia kati kuzifanyia ukaguzi wa kina kama zina uwezo wa kusafirisha abiria huku wakishauri kufufuliwa kwa Meli ya M.V Maendeleo.

Hadi hivi sasa ni meli moja tuu ambayo imekuwa ikifanya safari zake kisiwani Pemba baada ya Meli ya M.V Maendeleo nayo ilizuiliwa kutokana kuharibika injini moja.

Meli ya Serengeti imeanza kufanya safari zake baada ya kufanyiwa matengenezo kutokana na hapo awali kuwaka moto ikiwa katika maegesho ya bandarini.

Waziri Masoud, alisema msimamo wa Serikali hivi sasa ni kuzizuiya meli zote ambazo zinazofanya safari zake kwa kutumia injini moja kwa lengo la kuepusha kutokea kwa matatizo ya maafa hapo baadae.

Alisema tayari wameanza kulitekeleza hilo kwa kuizuiya meli ya MV Maendeleo, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kwa kutumia injini moja jambo ambalo ni hatari.

Alisema hapo awali baada ya Meli hiyo kuripotiwa juzi kuwa ilishindwa kwenda katika mwendo wake wa kawaida alifanya mazungumzo na uongozi wa meli hiyo na kumthibitishia ilikuwa na tatizo na aliamua kuizuia hadi itapofanya matengenezo.

Alisema alipata taarifa kutoka kwa Mrajis wa Meli kuwa tayari meli hiyo imeshatengenezwa na kuiruhusu kuendelea na safari zake.

Alifahamisha kuwa hivi sasa kumekuwa na tatizo la usafiri kwenda kisiwani Pemba kutokana na baadhi ya wafanyabishara wanaoendesha sekta ya usafiri baharini kutopendakupeleka boti zao kisiwani Pemba.

Hali hiyo Waziri Masoud alisema inakuja kutokana na wengi wa abiria wanaotumia usafiri wa Pemba ni wenye mizigo mizito huku kukiwa na idadi kubwa kiasi ambacho maboti hayo hayawezi kuhimili kutokana na viwango vyake.

Hata hivyo alisema suluhisho la matatizo hayo ni kuona Wizara hivi sasa inajipanga kuwa na boti zake zenyewe ambazo zitaweza kuendesha huduma ya usafiri kwa Unguja na Pemba hadi Dar es Salaam.

Serikali ya Zanzibar hadi sasa imekuwa ikimiliki Meli ya MV. Mapinduzi, MV Maendeleo ambazo husafirisha abiria na Meli ya Ukombozi inayofanya kazi ya kusafirisha mafuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.