Na Salum Vuai, Maelezo
BONANZA la pili la michezo linalohusisha wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari hapa Zanzibar, linafanyika asubuhi hii katika viwanja vya Maisara.
Tukio hilo adhimu litapata baraka za kufunguliwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa kamati inayosimamia bonanza hilo linaloandaliwa na Shirika la Magazeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kila kitu kuhusu tukio hilo kimekamilika.
Vyombo mbalimbali vya habari vya serikali na binafsi, vitashusha wachezaji wao wa michezo tafauti kuoneshana kazi ambapo zawadi nono kwa washindi zitatolewa.
Miongoni mwa taasisi hizo za kihabari, ni pamoja na waandaaji ambao ni gazeti la Zanzibar Leo, Habari Maelezo, Televisheni Zanzibar, Sauti ya Tanzania Zanzibar, Zenj FM, Coconut FM, Bomba FM, Chuchu FM, Hits FM, naVyuo vya Habari vya ZJMMC na MCC.
Aidha michezo ya soka, netiboli, riadha, mbio za mbatata, kula chapati na kunywa soda, kufukuza kuku, kukuna nazi na kuvuta kamba itarindima kuwapa wanahabari hao fursa ya kuonesha umahiri wao michezoni mbali na majukumu yao ya kuupasha habari umma.
Ratiba iliyotolewa na kamati ya bonanza hilo, inaonesha kuwa katika soka timu za Coconut FM na Sauti ya Tanzania Zanzibar zitakata utepe wa michuano hiyo ikiwa mechi ya kundi B.
Patashika za michezo hiyo zitaendelea hadi mchana na kuhitimishwa na mlo na vinywaji kwa washiriki na waalikwa wote, ambao kwa muda wote wa bonanza hilo watakuwa wakiburudishwa pia kwa muziki utakaopangiliwa na DJ maarufu Ali Ahmed Mcheju ‘Cool Para’.
Aidha mwisho wa bonanza hilo kutakuwa na utoaji zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali.
Bonanza hilo linafanyika chini ya udhamini wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), benki ya NMB, Zanzibar Bottlers, na pia kuchangiwa na hoteli ya Zanzibar Ocean View pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
No comments:
Post a Comment