Na Salum Vuai, Maelezo
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimemteua Ayoub Mohammed kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania ya umri wa chini ya miaka 23, inayojiandaa kwa michuano ya kufuzu fainali za Olimpiki mwaka 2012 nchini Uingereza.
Miohammed ambaye ni kocha wa klabu ya Chipukizi ya Pemba iliyo katika ligi kuu ya Zanzibar, amepewa mikoba hiyo kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF ) kuitaka ZFA iteue msaidizi wa Jamhuri Kiwelu ambaye ni kocha mkuu wa kikosi hicho.
Timu hiyo inajiandaa kwa mechi ya kusaka tiketi ya Olimpiki dhidi ya Cameroon mwezi ujao.
Mbali na uteuzi huo, ZFA kupitia kamati yake tendaji, imeshauriana na makocha Abdelfatah Abbas na Hemed Suleiman ‘Moroko’ kuona ni wachezaji gani wachaguliwe kujiunga na kambi ya timu hiyo ya Tanznia.
Tayari jopo hilo limewataja wanandinga 13 ambao miongoni mwao wamo walioshiriki michuano ya Chalenji ya vijana nchini Eritrea mwaka jana, pamoja na waliomo Zanzibar Heroes ambao hawajavuka umri huo.
Wachezaji hao na timu zao kwenye mabano ni Mahmoud Ali (Super Falcon), Mbarak Suleiman (Selem Rangers), Khamis Mcha na Amour Suleiman (Zanzibar Ocean View), Is-hak Othman na Salum Said (JKU), Gharib (Mtende), Saleh Hamad (Chuoni).
Wengine ni Abdulghani Gulam (Malindi), Vent Kamanya na Idrisa Abdulrahim (KMKM), Awadh Juma Issa (Taifa) pamoja na Abuu Omar kutoka Konde.
Wanasoka wote hao wametakiwa kuripoti kambini Dar es Salaam Machi 2, mwaka huu kuungana na wenzao 25 ambao kocha Jamhuri Kiwelu amewachagua kutoka klabu za Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment