Habari za Punde

ASKARI ALIYETEMBEZA KICHAPO JANG'OMBE APANDISHWA KIZIMBANI

Na Khamis Amani

ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kambi ya Bavuai Migombani, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shitaka la kuwashambulia raia huko Jang'ombe wiki iliyopita.

Askari huyo MT 83992 PTE, Emanual Elistile Ngondo (29) mkaazi wa Mombasa wilaya ya Magharibi Unguja, alifikishwa mbele ya hakimu Khamis Ali Simai wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, kujibu tuhuma za shambulio la hatari.

Shitaka hilo liliwasilishwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Said Mohammed Hemed, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika maelezo yake aliyoyatoa mahakamani hapo, Mwanasheria huyo alidai kuwa, Emanuel Elistile Ngondo, alimshambulia Ali Omar Ngasa kwa kumpiga mikwaju, magongo pamoja na mkia wa taa, tukio lililotokea Jang'ombe wilaya ya Mjini Unguja majira ya saa 9:00 za jioni.

Sambamba na tukio hilo, Mwanasheria huyo alidai kuwa siku hiyo ya Machi 9 mwaka huu, alimfunga Ali kwenye bomba la maji katika kambi ya Jeshi ya Bavuai iliyopo Migombani wilaya ya Mjini Unguja, na kumsababishia kupata maumivu makali mwilini mwake.

Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo wa serikali, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 225 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Mahakama ilipomtaka kujibu madai hayo ya upande wa mashitaka aliyakana na kuomba kupatiwa dhamana, ombi ambalo halikuwa na pingamizi mahakamani hapo.

Pamoja na kukana tuhuma hizo, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika, na kuomba tarehe ya kusikilizwa pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.

Kesi hiyo imeahirishwa kwa kusikilizwa hadi Machi 31 mwaka huu, na mtuhumiwa ametakiwa kujidhamini mwenyewe kwa fedha taslimu shilingi 50,000 pamoja na wadhamini wawili wenye vitambulisho, ambao kila mmoja ametakiwa kusaini bondi ya kiwango kama hicho cha fedha.

Hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani hapo jana, mtuhumiwa huyo alikuwa bado hajatekeleza masharti hayo ya dhamana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.